Michezo

Ushindi wa Manchester United wasababishia Leicester City kilio

July 27th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MANCHESTER United walijikatia tiketi ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao baada ya kuwalaza Leicester City 2-0 katika mechi ya mwisho wa msimu wa 2019-20 uwanjani King Power.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United walijibwaga ugani wakihitaji alama moja pekee kutokana na mchuano huo ili kujipa uhakika wa kutinga mduara wa nne-bora na hivyo kufuzu kwa soka ya UEFA muhula ujao.

Ni matokeo ambayo yaliishia kuwa ya kilio na kuvunja moyo wanasoka wa Leicester ambao walikuwa ndani ya mduara wa nne-bora kwa kipindi kirefu cha kampeni za msimu wa 2019-20.

Leicester walihitaji ushindi wa lazima dhidi ya Man-United pindi Chelsea walivyojipata uongozini dhidi ya Wolves uwanjani Stamford Bridge.

Hata hivyo, matumaini finyu ya kufuzu kwa Leicester yalizimwa na kiungo Bruno Fernandes katika dakika ya 71 kupitia penalti iliyochangiwa na tukio la Anthony Martial kuchezewa visivyo na nahodha Wes Morgan na beki Jonny Evans aliyeonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha pili kwa kumkabili kivoloya kiungo Scott McTominay.

Vikosi vyote viwili vilikuwa na fursa za kufunga huku kipa Kasper Schmeichel wa Leicester akilazimika kupangua makombora mawili ya Marcus Rashford katika kipindi cha kwanza naye Jamie Vardy akashuhudia mpira aliouelekeza langoni pa kipa David De Gea ukigonga mwamba wa goli.

Japo Leicester walitawaliwa na kiu ya kurejea mchezoni baada ya kufungwa bao la kwanza, masaibu yao yalizidishwa na tukio la Evans kufurushwa uwanjani. Kupungua kwa idadi yao kuliwapa Man-United motisha zaidi na wakafungiwa bao la dakika za mwisho kupitia kwa Jesse Lingard aliyetokea benchi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Leicester waliambulia hatimaye nafasi ya tano kwa alama 62 na hivyo kufuzu kwa soka ya Europa League msimu ujao.

Hata hivyo, kikosi hicho cha kocha Brendan Rodgers kilifutiwa machozi na ufanisi wa Vardy aliyeibuka Mfungaji Bora wa EPL msimu huu wa 2019-20 kwa jumla ya mabao 23, moja zaidi kuliko Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal na Danny Ings wa Southampton.

Hadi Fernandes alipowajibishwa kwa mara ya kwanza kambini mwa Man-United katika mechi iliyowakutanisha na Wolves mnamo Februari 1, 2020, kikosi cha Solskjaer kilikuwa katika nafasi ya nane jedwalini huku pengo la alama 14 likitamalaki kati yao na Leicester waliokuwa ndani ya mduara wa tatu-bora.

Kiungo huyo mvamizi mzawa wa Ureno alisajiliwa kutoka Sporting Lisbon kwa kima cha Sh9.5 bilioni.

Ujio wa Fernandes umekuwa kiini cha ufufuo wa makali ya Man-United ambao kwa sasa wameanza kuhisi ukubwa wa mchango wa kiungo Paul Pogba kila anapowajibishwa na Mreno huyo.