NA STANLEY NGOTHO
GAVANA wa Kajiado, Bw Joseph Ole Lenku, amesema ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ulikuwa wa haki na kwamba matokeo yake yaliakisi matakwa ya wakazi wa kaunti hiyo.
Gavana alisisitiza kuwa alimshinda mpinzani wake wa karibu Bw Katoo Ole Metito wa chama cha UDA – ambaye kwa wakati huu ni Msimamizi wa Ikulu – katika maeneo bunge matatu.
Aidha, alisema mgombea urais wa muungano wake wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, alipata kura nyingi katika kaunti hiyo huku Azimio ikishinda wadi 12 kati ya 25.
Akihojiwa wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya kupinga ushindi wake katika Mahakama ya Kajiado, jana Jumanne, Gavana Lenku alisema alizoa kura nyingi za ugavana katika eneobunge analotoka la Kajiado Kusini na lile la Kajiado Kaskazini.
“Nilipata ushindi huu kwa kura nyingi nilizozoa katika maeneo bunge matatu ya Kajiado Mashariki, Magharibi na Kati. Mgombea urais wa chama change pia alipata kura nyingi katika kaunti na pia ushindi katika viti vitatu kati ya vitano vya ubunge,” alisema Gavana Lenku.
Kesi ya kupinga ushindi wake imewasilishwa na Bw Paul Kerempu, mwalimu na mfanyakazi wa zamani wa serikali ya kaunti.
Subscribe our newsletter to stay updated