Habari MsetoSiasa

Ushirikiano mpya wa Obado na Ruto washutumiwa vikali

November 12th, 2018 1 min read

RUTH MBULA na VIVERE NANDIEMO?

BAADHI ya viongozi wamekosoa vikali ushirikiano mpya wa kisiasa kati ya Gavana wa Migori Okoth Obado na Naibu Rais William Ruto, licha ya gavana huyo kukabiliwa na kesi ya mauaji mahakamani.

Viongozi hao wamemlaumu Obado kwa kutumia ushirika huo kama kigezo cha “kukwepa” masharti ya mahakama.

Jana, viongozi kadha wa chama cha ODM katika eneo la Nyanza walieleza kukasirishwa na matamshi ya Bw Obado, wakiyataja kuwa “ya kipuuzi.”

Bw Obado amekuwa akiandamana na Bw Ruto katika hafla za kisiasa katika eneo la Nyanza Kusini, huku kauli zake zikikosolewa vikali na viongozi.

Jumamosi iliyopita, Bw Obado aliwaomba Wakristo kote nchini kumwombea, akifananisha hali inayomkabili na “kutembea motoni.”

Kando na hayo, alisema kwamba hali yake ni sawa na mtu aliyerushwa ndani ya kinywa cha mamba.

Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed alitaja matamshi hayo kama ukwepaji wa adhabu, akisema kuwa Bw Obado anajaribu kutumia siasa kuingilia kesi hiyo.

“Kwa kusema kwamba amerushwa katika kinywa cha mamba, anamrejelea nani? Wachunguzi au upande wa mashtaka?” akashangaa.

Wengine ambao wamejitokeza kukashifu kauli hiyo ni mwekahazina wa Kitaifa wa ODM, Bw Timothy Bosire na Mbunge Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Kisii, Bi Janet Ong’era.