Mazungumzo ya ushirikiano wa kisiasa ni jambo la kawaida – Mithika Linturi

Mazungumzo ya ushirikiano wa kisiasa ni jambo la kawaida – Mithika Linturi

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Meru Mithika Linturi amekubali kuwa kuna uwezekano kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya kambi za chama cha United Democratic Alliance (UDA) na Amani National Congress (ANC) kuhusiana na uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiongea katika kipindi cha mahojiano ya kisiasa katika runinga ya Citizen, Jumatatu asubuhi, Bw Linturi hata hivyo alisema huenda kuna wabunge wanaoendesha mazungumzo hayo bila ufahamu wa vinara wa vyama hivyo.

“Siwezi kukana wala kukubali kwamba mazungumzo kama hayo yanafanyika. Lakini ifahamike kuwa mikutano kama hiyo, ya kisiri, inatarajiwa kufanyika wakati kama huu ambapo uchaguzi mkuu unakaribia,” Bw Linturi akasema.

Japo kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi amepuuzilia mbali madai kuwa anafanya mazungumzo na Naibu Rais William Ruto, madai yameibuka kwamba wabunge wa chama chake wamekuwa wakishauriana na wenzao wanaoegemea UDA.

Duru zasema kuwa mazungumzo hayo yanalenga kumwezesha Bw Mudavadi kushirikiana na Dkt Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Naibu kiongozi wa ANC Ayub Savula, Jumapili alinukuliwa akisema kuwa kuna viongozi wa chama hicho wanaoendesha mazungumzo hayo.

Aidha, alidai kuwa baadhi ya viongozi hao wa ANC wamehongwa kusudi watumike kama maajenti wa Dkt Ruto katika eneo la Magharibi mwa Kenya.

Bw Savula alifichua kuwa Seneta Cleophas Malala ndiye anaongoza njama ya kumsukumu Bw Mudavadi kufanya kazi na Dkt Ruto.

Hata hivyo, Bw Malala amekana madai ya Bw Savula akisema hayana mashiko wala ukweli wowote.

“Siwezi nikajibu madai ya Savula kwa sababu ni porojo na hayana maana yoyote,” akasema, kuashiria kuna mgawanyiko mwingine ndani ya ANC.

Bw Mudavadi pia alikana madai kuwa baadhi ya wabunge wa chama chake wamekuwa wakihongwa ili kumshinikiza abuni muungano na Dkt Ruto.

“Je, ulishuhudia ama unauliza kuhusu uvumi? Ikiwa mtu atafikishwa mahakamani kuwajibikia hilo je, utajiwasilisha kama shahidi? Nijuavyo ni kwamba hakuna mipango kama hiyo,” akawaambia wanahabari baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki la St Jude Thaddeus katika mtaa wa Huruma, Kaunti ya Uasin Gishu.

Lakini Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amefichua kuwa vinara wawili wa OKA ambao hakuwataja majina wamekuwa wakifanya mazungumzo na Naibu Rais Dkt Ruto.

Bw Barasa alisema vinara hao wa OKA humtembelea Naibu Rais kwa kile alichokitaja kama, “mashauriano ya kisiasa”.

“Ningetaka kisisitiza kuwa sio wabunge pekee ambao hukutana na Dkt Ruto kwa mashauriano, bali pia vinara wawili wa OKA. Wao humtembelea Naibu Rais usiku kufanya mashauriano ya kisiasa bali sio kwa ajili ya kupokea hongo,” mbunge huyo akanukuliwa akisema.

Wiki jana, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli pia alidai kuwa Dkt Ruto amekuwa akiwahonga wabunge fulani kutoka Magharibi ili kuvuruga juhudi za kuleta umoja wa kisiasa eneo.

You can share this post!

Washirika wa Ruto wadai Obado avuruga chama cha Naibu Rais

Corona: Afrika Kusini sasa yadai ‘kuonewa’

T L