Makala

Ushirikina wazidi kutesa jumuiya ya Kikristo

July 27th, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

WACHUNGAJI wa Kikristo wameduwazwa na jinsi wafuasi wao wengi wamejiunga na itikadi za ushirikina ambapo wamepoteza imani ya kusuluhisha changamoto zao za kimaisha kupitia maombi na badala yake kuweka imani yao kwa uchawi.

Wanasema imani hiyo ya uchawi inavuma kwa nguvu miongoni mwa Wakristo na ni hatari kwa maagizo na amri za dini hiyo.

Makachero katika Kaunti ya Murang’a kwa sasa wanafuatilia mienendo ya dhehebu moja la Akorino kuhusu visa vya utekaji nyara na mauaji ya kafara dhidi ya watoto.

Makachero hao wanateta kuwa hafla hizo za ‘uchawi’ miongoni mwa wafuasi wa dhehebu hilo ni hatari kwa usalama wa eneo hilo kwa kuwa wazazi tayari wamejawa na hofu.

Kwa mujibu wa afisa anayeongoza uchunguzi huo Bi Gad Kinoti, kisa kinachofuatiliwa ni cha mvulana ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya chekechea na ambaye aliripotiwa kutoweka kutoka kijiji cha Gathiru lakini siku mbili baadaye mwili wake ukapatikana ukiwa na majeraha katika sehemu za siri, shingo na tumboni.

“Hali hii kwa uchunguzi wa msingi inaonyesha mauaji ya kidini ndani ya msukumu wa ushirikina,” Gad Kinoti akaambia Taifa Leo.

Padri Joseph Wamalwa wa Kanisa katoliki kutoka Kaunti ya Nairobi anateta kuwa ishara za ushirikina kuvuma miongoni mwa Wakristo ni jinsi visa vinavyovuma vya washukiwa wa ukora hulishwa nyasi kila kuchao, sehemu za siri kunyofolewa kiholela na pia mauaji dhidi ya zeruzeru huku Wakristo wengi wakinaswa wamevalia hirizi kujikinga dhidi ya mikosi ya ama kijamii, kiuchumi au kisiasa.

“Ni mtindo ambao umekuwa ukishuhudiwa miongoni mwa wafuasi wanaoamini desturi za Wakristo lakini sasa umefika mahali ambapo umezua taharuki ya kuonyesha jinsi imani halisi inayumbishwa. Ni wazi kuwa tuko na janga la kuabudu uchawi kama kinga na hali hii inavuma sana Afrika. Lakini hatari iliyoko ni kuwa wanaoamini uchawi au kutafuta huduma zake kwa minajili yoyote wataukosa Ufalme na sio siri,” anasema.

Ili kuelimisha jamii kuhusu madhara ya kuamini mambo ya uganga na uganguzi wa juju, George Ongere ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Center for Inquiry-Kenya anasema wameandaa mikakati ya kuandaa warsha kote nchini kupambana na nguvu za giza.

“Tumepanga mikakati ya miezi mitano inayobakia mwaka huu kuelimisha Wakenya kuhusu athari za kushikilia misimamo ya ushirikina,” anasema.

Kupitwa na wakati

Anasema mikakati hii imeanzishwa katika Chuo Kikuu cha Moi ambapo kikundi kiitwacho Moi Freethinkers kwa sasa kiko mstari wa mbele kuhamasisha wananchi dhidi ya kuamini mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati.

“Hatua kama hiyo inashirikishwa na kikundi kingine kutoka chuo kikuu cha Nairobi. Kuwatumia wanafunzi wa vyuo vikuu kuna maana kuwa tutapata waelimishaji ambao wana umakinifu wa mawazo ya kisasa,” anasema.

Aidha, Ongere anasema kuwa wameanzisha jarida liitwalo Skeptical Inquirer, ambalo ni la kupeanwa bure kwa raia ili wajisomee mijadala ya kuunga na kupinga mila na desturi zinazoambatana na ushirikina.

Kama dhihirisho wazi kuwa ripoti hiyo ina ukweli mzito, Kanisa Katoliki katika Kaunti ya Embu tayari imetangaa vita dhidi ya mapadri na waumini ambao huamini itikadi za ushirikina.

Katika vita hivyo, lilitangaza kuwa tayari limemtimua padri mmoja katika Parishi ya Kamiruri baada ya uchunguzi kubainisha kuwa alikuwa akitembelea manabii na washirikina kutatuliwa s hida zake za kimaisha.

Padri Naziel Mugo akitoa taarifa hiyo alisema kuwa kwa muda kanisa hilo limekuwa likifanya uchunguzi wake kuhusu kukumbatiwa kwa ushirikina na mapadre na waumini wake na kupata ukweli wa kushtusha.

“Wengi wa waumini wamekumbatia itikadi za kuwaendea manabii na wachawi kupata huduma za kutatua shida zao. Wengi wamekili kuwa wamekuwa wakiuziwa huduma hizo, baadhi yao hata wakisema walikuwa wakitafuta huduma za kuwaharibu mahasidi wao,” akasema.

Ni hivi majuzi ambapo mwanamume mmoja ambaye ni baba wa watoto wanne aligonga vichwa vya habari katika kaunti hiyo, baada ya kutangaza hadharani kuwa sehemu zake za siri zilikuwa zimetoweka baada ya kutekelezewa ushirikina na mkewe.

Ilibidi mapasta wawili waitwe kutoka Kaunti ya Nairobi kumwombea ili viungo vyake vya mwili virejee mahala pake.

Bw Mugo alisema kuwa imani ya dini Katoliki haikubali misukumo ya aina hiyo katika maisha ya binadamu, kuwa msimamo wao ni kumuomba Mola awajalie waliosoneneka kimaisha rehema za roho mtakatifu.

Alisema kuwa waumini wote wa Kikristo wanafaa kukaa imara katika neno la Mungu na wafahamu kuwa yote ambayo huwakumba maishani, mema au mabaya huwa na sababu na afueni za baraka ni za kutoka kwa Maulana mwenyewe ila sio kwa washirikina na manabii wa uongo.

“Sioni Mkristo akisaidika baada ya kuuziwa maji ya mtoni akidanganywa kuwa ni maji matakatifu. Matakatifu baada ya kubarikiwa na nani? Mbona Mungu atujalie maji ya kunywa kutoka kwa mvua, visima na mabwawa lakini ya kubariki watu yawe mikononi mwa washirikina?” akahoji.

Katika Kaunti jirani ya Murang’a, wakazi wa maeneo kadha tayari wamezindua mikakati ya usalama ya kuwakinga dhidi ya wachawi.

Katika Kijiji cha Githiga, wenyeji wamesema kuwa kuwa hatua hiyo iliafikiwa baada ya kuripotiwa visa vya washukiwa wa uchawi kujipenyeza miongoni mwao wakisingizia dini ya Unabii na Utabiri wa maisha ya wenyeji.

Juhudi hizo zitashirikishwa na chifu wa eneo hilo Bw Samuel Karuma ambaye alisema kuwa ni jukumu la wenyeji kujikinga dhidi ya athari za ushirikina.

“Katika mpango huu wa wenyeji, kila kanisa geni litapigwa msasa kuhusu maadili na mitazamo ya imani yake haswa kwa zile ambazo huandaa krusedi tu bila kuwa na mahali maalumu pa ibada,” akasema.

Aidha, wenyeji watawajibika katika kufuatilia mienendo ya wafuasi wa madhehebu ambayo huzua shaka katika mienendo na injili zao.

Alisema kuwa hatua hiyo ilichochewa na kisa cha wiki jana ambapo wanawake wawili wa miaka 20 kila mmoja walivamiwa na wenyeji wa kijiji hicho baada yao kuzindua matembezi ya boma hadi lingine wakitoa utabiri wa kushtusha wenyeji.

“Wawili hao waliishia kulazwa katika hospitali kuu ya Kaunti ya Murang’a wakiwa hali mahututi. Ingawa wasichana hao walikuwa wakijifanya wahubiri, walipatikana na vifaa vinavyohusishwa na ushirikina ikiwemo nyoka kubwa vikiwa katika mikoba yao,” akasema Bw Karuma.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, wafanyabiashara wamekuwa wakitekeleza visa vya kustusha katika maduka yao ambapo wamekuwa wakiwasajili wachawi kutoka Kaunti za Pwani, Meru na Nyeri ili kuyaganga dhidi ya wezi.

Mwanamke mmoja ambaye ni muuzaji wa mchele anasema “mimi ni Mkristo na hujikinga dhidi ya wezi wa mali yangu kupitia uchawi.”

Anaongeza: “Juzi tuliungana tukiwa wafanyabiashara 100 na tukawaleta waganga watano ili kutulinda dhidi ya wavamizi wa mali yetu. Aidha, walituhakikishia kuwa hata tukipeleka mamilioni kwa benki, tusiwe na hofu kwa kuwa tumekingwa na nguvu za uchawi dhidi ya majambazi na matapeli.”

Majuzi, Kaunti ya Embu ilirejea katika vichwa vya habari baada ya ‘Mkristo’ mwingine kunaswa na vifaa vya uchawi ambavyo alikuwa amebandika katika kibanda chake cha kuuzia mboga na matunda.

Aliposukumwa na wenyeji aelezee ni kwa nini alikuwa ametekeleza uchawi miongoni mwa Wakristo wenzake, alinuna akisema kuwa wengi wa wafanyabiashara katika soko hilo huwa na ulinzi wa hirizi za ushirikina, na hakuona lolote la kushangaza.

Alisema kuwa aliamua kwendea huduma za wachawi kufuatia msururu wa kuibiwa mali zake ndani ya soko hilo.

“Kwa kipindi cha miezi sita, nimepoteza jumla ya Sh120,000 kutoka biashara yangu baada ya kibanda changu kuvunjwa na hatimaye mali na pesa taslimu kuibwa. Niliamua kujikinga na nguvu za ushirikina kwa kuwa wakuu wa soko na pia maafisa wa polisi hawanipei suluhisho,” akasema.