Kimataifa

Ushoga ni zawadi yangu kutoka kwa Mola, mkuu wa Apple asema

October 25th, 2018 1 min read

CNN na PETER MBURU

New York

Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa kampuni ya kutengeneza simu na kompyuta ya Apple Inc Bw Tim Cook amekiri kuwa hali yake ya kuwa shoga ndiyo zawadi kubwa zaidi aliyompa Mungu.

Bw Cook alisema anafurahia hali yake na uamuzi aliofanya wa kutangaza wazi kuhusu hali yake, miaka minne baada ya kuja mbele ya umma kutangaza kuwa yeye hujihusisha na mapenzi ya mume kwa mume.

“Ninajivunia sana hali yangu,” Bw Cook akasema katika mahojiano na mtangazaji wa CNN Christiane Amanpour Jumatano. Alisema kuwa shoga “ndiyo baraka kubwa sana ya Mungu kwangu.”

Mnamo Oktoba 30, 2014, Bw Cook alitangaza wazi kuwa alikuwa shoga, baada ya muda mrefu wa watu kukisia hali hiyo.

“Nilitangaza wazi kwa kuwa nilianza kupokea jumbe kutoka kwa watoto waliosoma mitandaoni kuwa nilikuwa shoga,” akaeleza Bi Amanpour.

Alisema kuwa jumbe hizo zilitoka kwa watoto waliosema kuwa walikuwa wamenyanyaswa kwa kutangaza hali yao ya kimapenzi.

Alisema kuwa uamuzi wake ulinuia kuwapa motisha watoto wadogo kuwa bado “wanaweza kuwa mashoga na wafanye kazi kubwa maishani.”

Alisema kutangaza hivyo kulimsaidia kama kiongozi.

Alisema hata watu ambao wamekuwa wakipinga hali yake wazi wamemsaidia kuwa shujaa kwa kuwa amefahamu umuhimu wa kuwa katika kikundi cha watu wachache na ambao sharti wateteane.