Habari

Ushoga: Wazee kutakasa Mlima

December 30th, 2019 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

WAZEE wamepanga kufanya maombi maalumu kutakasa Mlima Kenya, wakidai ulichafuliwa wakati makundi ya mashoga yalipopandishia bendera yao hivi majuzi.

Baraza la Wazee wa jamii ya Wakikuyu lilisema litakapoandaa maombi ya kufunga mwaka kesho Jumanne katika uwanja wa michezo wa Nanyuki, mojawapo ya masuala yatakayoombewa ni kutaka Mungu atakase mlima huo unaoaminika na jamii hiyo kuwa umetendewa najisi.

Katibu Mkuu wa baraza hilo, Mzee Peter Munga, alisema mlima huo ni mtukufu na haustahili kutendewa vitendo visivyokubalika katika jamii.

Aliongeza kuwa watalazimika kutafuta watu watakaoukwea ili wakaondoe bendera hiyo ya ushoga.

“Tunataka utakaso kwa sababu mlima huo ni mtukufu. Sisi hatufuati imani za makundi hayo kwani yale wanayofanya ni ya laana,” akasema.

Hivi majuzi, makundi ya kutetea haki za kibinadamu na wanachama wa kikundi cha mashoga na wasagaji walikwea Mlima Kenya na kutundika bendera yao.

Walisema uamuzi wao wa kukwea mlima huo ulilenga kutoa hamasisho kuhusu mpango wanaoendeleza wa kuchangisha pesa za kujenga nyumba itakayotumiwa kuficha watetezi wa haki za kibinadamu wanapokuwa hatarini.

Mzee Munga aliongeza kwamba, kutokana na kuwa wazee hawana nguvu za kukwea mlima huo, huenda wakalazimika kutafuta vijana waende wakang’oe bendera hiyo.

“Tutatafuta watu waende wakaondoe bendera hiyo,” akasema.

Mbali na hayo, wazee hao wamepanga pia kutoa ratiba yao ya kuhamasisha jamii kuhusu ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) hapo kesho. Baraza hilo ambalo linaegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, lilisema litaeleza yale ambayo wangependa yafanyiwe marekebisho katika ripoti hiyo.

“Tutahamasisha umma kuhusu mabadiliko yanayostahili kufanywa kupitia kwa kura ya maamuzi, ambayo si ghali jinsi baadhi ya wanasiasa wanavyotaka tuamini,” akasema Bw Munga.

Wabunge wa Mlima Kenya wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, almaarufua Tangatanga, walikuwa tayari wametoa ratiba yao ya kuhamasisha umma kuhusu ripoti hiyo kuanzia Januari 7. Miongoni mwa mabadiliko ambayo wazee wa jamii hiyo wanataka ni marekebisho katika mfumo wa kugawa fedha kwa kaunti na maeneobunge.

Wanataka ugavi uwe ukifanywa kwa kuzingatia idadi ya watu.

Katika mkutano wao wa Nanyuki, wazee hao pia wanatarajiwa kutangaza msimamo kuhusu ziara ya kikundi cha wazee wengine wa jamii hiyo kutoka Rift Valley ambao walimtembelea Dkt Ruto nyumbani kwake Sugoi, wakiongozwa na Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri.

Bw Munga alisema baraza lao la wazee halina pingamizi dhidi ya mgombeaji yeyote wa urais akiwemo Dkt Ruto, bali wanachopinga ni kiongozi yeyote kuenda kumwahidi kwamba jamii itamuunga mkono kisiasa.

“Mgombeaji yeyote aliye na uwezo wa kuongoza nchi kwa uaminifu yuko huru kuomba kura za jamii ya Agikuyu ambazo ni takribani milioni saba. Wako huru kushauriana na jamii lakini lazima watueleze tutanufaika vipi katika serikali baada ya 2022,” akasema.

Alimkosoa Dkt Ruto kwa kutumia “watu wasiofaa” kumtafutia umaarufu Mlima Kenya badala ya kufanya hivyo kupitia kwa Rais Kenyatta na wazee wa jamii.

Kulingana naye, hatua hiyo ambayo anasema imesababisha mgawanyiko kati ya makundi ya Kieleweke na Tangatanga eneo hilo, inaweza kufasiriwa kama hatua ya Dkt Ruto kumkosea Rais heshima.