Ushonaji mikeka waokoa wanawake kiuchumi Lamu

Ushonaji mikeka waokoa wanawake kiuchumi Lamu

NA KALUME KAZUNGU

IDADI ya wanawake wa jamii ya Wabajuni katika vijiji vya Kaunti ya Lamu ambao wanajitosa kwenye kazi za kushona vikapu na mikeka inaongezeka, wengi wakijisakia mbinu za kujipa fulusi za kukabili gharama ya juu ya maisha.

Bi Khadija Abubakar, ambaye ni mkazi wa Matondoni, anasema yeye hupata hadi Sh30,000 kwa mwezi mmoja kupitia kwa ushonaji wa vikapu na mikeka.

Kulingana naye, biashara hiyo imemwezesha kusaidiana na mumewe kugharimia mahitaji ya familia yao katika jamii ambapo familia nyingi hutegemea mapato ya mume pekee.

Mama huyo wa watoto sita alianza ushonaji wa mikeka na vikapu baada ya mumewe ambaye ni mvuvi kuanza kulalamika jinsi sekta yao ilivyoathiriwa na miradi ya kujenga miundomsingi kama vile bandari ya Lamu.

Baadhi ya maeneo ambayo wavuvi walitumia awali kutekeleza shughuli zao yaliharibiwa na ujenzi wa bandari.

Kulingana na Bi Abubakar, mkeka mmoja huuzwa kwa kati ya Sh800 na Sh1,000 kwa mnunuzi wa kawaida. Kwa mtalii, bei huwa tofauti kwani yeye huuza mkeka kwa kati ya Sh3,500 hadi Sh5000.

“Nashukuru kwa kazi hii ya kushona mikeka na vipaku. Awali, tulikuwa tukimtegemea mume wangu kukimu kila hitaji la familia. Hiyo ilimletea msongo wa mawazo. Hata nyumbani kulikosekana amani kinyume na ilivyo sasa,” akasema Bi Abubakar.

Bi Sharifa Athman, mkazi wa Pate, anasema mbali na kuleta fedha nyumbani, ushonaji wa vikapu na mikeka pia umesaidia kuleta umoja kati ya mke na mume.

Bi Athman anasema wanaume wengi siku hizi wameanza kujiunga na wake wao kushona mikeka pamoja na kuuza, hivyo kuongeza faida nyumbani.

“Upendo wa bibi na bwana umeongezeka kupitia ushonaji wa mikeka. Siku hizi mabwana wakikosa kwenda baharini kuvua samaki, wao hujiunga nasi kushona vikapu na mikeka. Hii imechangia kuleta ukaribu na mahaba kati ya mume na mke. Tunashukuru kazi ya kushona sasa imekuwa kiokozi kwa wanandoa,” akasema Bi Athman.

Bw Mohamed Shee, mkazi wa kisiwa cha Kiwayu, Lamu Mashariki, alikiri kuwa ushonaji wa mikeka na vikapu umechangia kustawi kwa familia kwani kila mmoja anawajibikia utunzaji wa familia badala ya majukumu hayo kuachiwa wanaume pekee.

“Kitambo wanawake wetu walikuwa wakikaa tu nyumbani kusubiri sisi mabwana kujukumikia mahitaji yote ya familia. Wao lao lilikuwa jikoni na kuzaa. Twashukuru uwajibikaji wa mabibi zetu umeleta amani kudumishwa majumbani. Hata talaka zimepungua,” akasema Bw Shee.

Afisa Mtendaji wa Shirika la Wanawake la Lamu Women Alliance (LAWA), Bi Raya Famau, aliwapongeza wanawake kwa kuibua mbinu ya kushona mikeka na vikapu hivyo kuleta mchango katika uendelezaji wa ndoa na familia.

“Nafurahi kwamba leo kina mama wa Lamu hawasubiri mabwana zao walipe karo ya watoto shuleni, kununua chakula nyumbani na ununuzi wa nguo. Wao wamejituma katika kazi zao na kujipatia fedha za kukimu mahitaji yao wenyewe na pia ya kifamilia,” akasema Bi Famau.

  • Tags

You can share this post!

Wasomi waanza kupigania uvaaji wa hijab shuleni

Ndani ya himaya ya ‘Yesu wa Tongaren’

T L