Michezo

Ushuru FC wazimwa na Talanta

May 7th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MATUMAINI ya Ushuru FC kupiga hatua kwenye kampeni za kipute cha Supa Ligi ya Taifa (NSL) yaligongwa mwamba ilipopigwa mabao 2-1 na FC Talanta uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Nayo Kisumu Allstars iliendelea kukaa kileleni licha ya kutoka sare tasa dhidi ya Bidco United kwenye patashika iliyopigiwa Thika Stadium mjini humo.

Chris Owino aliiweka Talanta FC kifua mbele dakika ya 36 kabla ya Job Tinyo kuongeza la pili dakika 22 baadaye.

Hata hivyo dakika ya 69, Brian Yakhama alitingia Ushuru bao la kufuta machozi. ”Tulikubali yaishe maana tuliteleza wapinzani wetu walipotangulia kufunga,” kocha wa Ushuru, Ken Kenyatta alisema.

Naye kocha wa FC Talanta, Abdalla Juma alishukuru vijana wake kwa kujitahidi na kuzoa ushindi wa alama zote mbele ya ushuru FC.

”Hakika napongeza wachezaji wangu kwa kazi wanaofanya maana bado hatujayeyusha matumaini ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya KPL msimu ujao,” alisema.

Nayo Nairobi Stima ilitwaa bao 1-0 dhidi ya St Josephs Youth na kulipiza kisasi baada ya kulazwa mabao 2-1 na Shabana FC wiki iliyopita. Kwenye msimamo wa ngarambe hiyo, Ushuru imeshuka na kutua nafasi ya nne kwa alama 59 tatu mbele ya Kenya Police.

Kwa kufikisha alama 64 Kisumu Allstars ingali kidedea, Nairobi Stima ndiyo ya pili kwa kuzoa pointi 60, moja mbele ya Wazito FC. Kwenye mechi hizo, Migori Youth ilinyukwa mabao 5-0 na Green Commandos nayo Shabana FC iliagana bao 1-1 na Modern Coast Rangers.