Michezo

Ushuru FC yaangusha Josephs Youth Academy

September 2nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MWANASOKA shupavu Jackton Opanda amecheka na wavu mara moja na kubeba Ushuru FC kunyuka Josephs Youth Academy goli 1-0 kwenye mechi kali ya Supa Ligi ya Taifa (NSL) iliyopigiwa ugani Ruaraka, Nairobi.

Ushuru FC chini ya kocha, James ‘Odijo’ Omondi aliyekuwa akifunza Muhoroni Youth ilipata ushindi baada ya kujaza kimiani bao hilo dakika ya 82.

”Ni furaha tele kuanza muhula mpya kwa ushindi hasa kwenye mechi iliyoshuhudia ushindani wa kufa mtu. Inashiria wazi kuwa nina kikosi imara ila tunahitaji kujipanga vyema ili kufanya kweli,” alisema kocha huyo anayelenga kutwaa tiketi ya kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Pia alidai alipania ushindi mnono ila aliteleza baada ya kukosa huduma za wanasoka wanne muhimu akiwamo: Brian Yakhama, Evans Maliachi, David Mwangi na Brian Okeyo.

Naye Dennis Wafula alipiga ‘Hat trick’ na kusaidia Vihiga United iliyoshushwa daraja msimu uliyopita kubugiza Migori Youth magoli 3-1 kwenye patashika iliyosakatiwa Mumias complex, mjini humo. Migori Youth ilipata bao la kufuta machozi kupitia Edward Odhiambo.

Nao washiriki wapya, Vihiga Bullets ilianza kampeni zake vibaya ilipozabwa mabao 3-1 na FC Talanta Uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Kwenye matokeo mengine, Nairobi Stima ilikandamiza Northern Wanderers kwa magoli 8-0 huku Bidco United ya kocha, Leonard Saleh ikizoa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mt Kenya United.