Michezo

Ushuru na Wazito washuka NSL

April 15th, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Ushuru na Wazito FC zimeteremka kwenye msimamo wa Supa Ligi (NSL) baada ya kupoteza mechi zao za mwishoni mwa wiki. Ushuru wameshuka hadi nafasi ya tatu, wakifuatiwa na Wazito.

Huku kila timu ikiwa imebakisha mechi 12, Kisumu All Stars wamechukua usukani jedwalini baada ya kujibwaga uwanjani mara 26, wakifuatiwa na Nairobi Stima ambao walitoka sare 1-1 na Green Commandos mjini Naivasha.

Ushuru walichapwa 2-1 na Shabana ugenini ugani Gusii na kuteremka hadi nafasi ya tatu wakati Wazito wakininginia katika nafasi ya nne kwenye msimamo huo. Ushindi wa Shabana umewarusha kutoka nafasi ya 10 hadi ya tisa jedwalini.

Licha ya kuibuka na ushindi wa 2-1 uwanjani Hope Centre, Nairobi City Stars waliendelea kubakia katika nafasi mbaya pamoja na Thika United ambao wameshindwa kutumia ujuzi wao kuandikisha matokeo mema msimu huu.

FC Talanta 3 Fortune Sacco 3; Nairobi City Stars 2 Modern Coast Rangers 1, Coast Stima 5 Kanagemi All Stars 2; Eldoret Youth 2 Wazito 1; Administration Police 2 Thika United 2; St Joseph Youth 0 Kenya Police 1; Kisumu All Stars 2 Migori Youth 0; Shabana 2 Ushuru 1; Nairobi Stima 1 Green Commandos 1.