Ushuru wa juu, madeni yachangia bei za juu za mafuta

Ushuru wa juu, madeni yachangia bei za juu za mafuta

Na BENSON MATHEKA

KUPANDA kwa bei za mafuta nchini kumesababishwa na viwango vya juu vya ushuru, kupanda kwa bei za bidhaa hiyo kimataifa na madeni ambayo serikali imelimbikizia nchi.

Wataalamu wa uchumi wanasema kuwa, ushuru unaotozwa mafuta nchini ni wa juu mno ikilinganishwa na nchi jirani ambako bei za bidhaa hiyo ni nafuu.

Kwa kila lita ya mafuta, Sh67 huwa ni ushuru, jambo linalochangia bei kuwa za juu.Kulinmafuta

gana ripoti ya hali ya uchumi ya Shirika la Taifa la Takwimu (KNIBS), bei za mafuta nchini zimekuwa zikiongezeka kutokana na ongezeko ya bei katika ngazi ya kimataifa.

Ripoti inasema kwamba bei zitaendelea kuongezeka katika miezi iliyosalia mwaka huu na kuathiri ukuaji wa uchumi.“Bei za mafuta zimekuwa zikiongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na kupanda kwa bei kimataifa.

Kwa wastani, bei za mafuta kimataifa zinatarajiwa kuwa zaidi ya asilimia 50 mwaka wa 2021 ikilinganishwa na 2020. Matokeo yatakuwa bei za mafuta nchini Kenya kuendelea kupanda na kulemaza ukuaji wa uchumi,” inasema ripoti hiyo.

Kulingana na mwanauchumi Kwame Owino, Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Masuala ya Uchumi (IEA), ushuru wa hali ya juu unaopendekezwa na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) kama sharti la kuipa Kenya mikopo, pia umechangia kupanda kwa bei za mafuta nchini.

Serikali imekuwa ikikopa pesa kutoka IMF kufadhili sehemu ya bajeti yake na haina budi kutimiza masharti ya shirika hilo ambayo huwa yanaumiza raia wanaolazimika kutozwa kodi zaidi.

Bw Owino anasema wabunge pia walichangia kuongezeka kwa bei za mafuta kupatia sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) inayopatia shirika hilo jukumu la kuamua bei za mafuta jambo ambalo liliondoa ushindani.

Shirika hilo la serikali, huwa linachunguza bei za mafuta kila baada ya mwezi mmoja na kutangaza mpya kwa kutengemea bei za kimataifa.

“Hatua ya kuthibiti bei za mafuta iliondoa ushindani. Kampuni za mafuta zingeachwa kushindana na hii ingefanya bei kuwa nafuu,” asema Bw Owino.

Anasema licha ya hayo, bei za mafuta kimataifa huwa zinategemea thamani ya dola la Amerika dhidi ya sarafu ya nchi husika.

“Thamani ya dola ikiwa juu kuliko sarafu ya nchi husika, bei ya mafuta, bima na uchukuzi huwa zinaongezeka pia. Kwa muda sasa, thamani ya shilingi ya Kenya imekuwa hafifu dhidi ya dola ya Amerika,” Bw Owino aliambia Citizen Tv.

You can share this post!

Miaka 10 ndani yamsubiri Wario kwa ufisadi

Bei: Wakenya waishiwa pumzi