Michezo

Ushuru yarejea kileleni NSL

April 8th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Nairobi Stima iliichabanga Fortune Sacco kwa magoli 3-1 nao wanasoka wa Ushuru FC walipiga tatu safi na kurukia uongozi wa kinyang’anyiro cha Supa Ligi ya Taifa(NSL) msimu huu.

Ushuru FC ya Kocha, Ken Kenyatta ilivuna pointi tatu muhimu ilipoangusha Thika United mabao 3-0 kwenye mechi safi iliyosakatiwa uwanja wa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Nayo Wazito ilijipata hoi na kubanduliwa kileleni ilipodunga bao 1-0 na Shabana FC. Wachezaji wa Ushuru walijipatia mafanikio hayo kupitia Evans Maliachi, Alex Sunga na Patrick Macharia baada ya kila mmoja kutikisa wavu mara moja.

”Tunashukuru kwa kila hatua maana tunazidi kukaza buti,” kocha wa Ushuru alisema.

Juhudi za Ushuru kurejelea mechi za Ligi Kuu nchini ziligonga mwamba mara mbili kunako dakika za mwisho, mwaka 2017 na 2018 imekuwa ikibanduliwa katika fainali baada ya kushushwa ngazi mapema 2017.

Nayo Kisumu Allstars iliangusha Kangemi Allstars kwa mabao 2-0 na kuendelea kufunga tano bora, huku Sanneh Ebrimah akipiga mbili safi na kubeba Nairobi City Stars kukung’uta Coast Stima kwa mabao 2-1.

Kwenye mechi hizo, Kibera Black Stars ilibanwa kwa bao 1-0 na Eldoret Youth, Green Commandos ilitoka nguvu sawa mabao 2-2 na Administration Police (AP) huku Kenya Police ikibeba matokeo sawa na hayo dhidi ya FC Talanta.

Ushuru iko kifua mbele kwa alama 52 sawa na Nairobi Stima tofauti ikiwa idadi ya mabao.