Michezo

Ushuru yashuka, Wazito wapaa NSL

April 29th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Nairobi Stima ilichomwa kwa mabao 3-1 na Ushuru FC wakati Kisumu Allstars ikirukia uongozi wa kipute cha Supa Ligi ya Taifa (NSL) baada ya kubeba mabao 2-1 mbele ya Shabana FC kwenye patashika iliyosakatiwa uwanja wa Gusii Stadium mjini Kisii.

Nao wanasoka wa Wazito FC walishuka hatua moja licha ya kubamiza Coast Stima kwa mabao 4-3 kwenye mechi iliyopigiwa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi. Shabana FC ilitwaa uongozi wa mchezo huo kunako dakika ya 24 kupitia bao lililotingwa na John Musyoka licha ya kusalia la kufuta machozi baada ya dakika tisini kukatika.

Kipindi cha lala salama wachezaji wa Kisumu Allstars warejea dimbani kivingine na kusawazishiwa na Moses Okumu kabla ya Shadrack Omondi kuitingia bao la ushindi dakika ya 60. Matokeo hayo yameashirua wazi kwamba mambo ni magumu wala hakuna kulaza damu.

Matokeo hayo yameiweka Kisumu Allstars kidedea kwa kufikisha alama 60, sawa na Wazito FC tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nayo Ushuru inayoshiriki kipute hicho kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kushushwa inafunga tatu bora kwa kufikisha pointi 59, nne mbele ya Nairobi Stima ikifuatiwa na Kenya Police.

Kwenye matokeo ya mchezo mwingine, kikosi cha Kangemi Allstars kilicharaza Fortune Sacco mabao 3-1, St Joseph ilinyukwa mabao 2-1 na Thika United wakati Migori Youth ilitoka bao 1-1 na Kenya Police.

MATOKEO YOTE MECHI ZOTE WIKENDI

Wazito FC 4-2 Coast Stima

Administration Police (AP) 1-3 FC Talanta

Ushuru 3-1 Nairobi Stima

Fortune Sacco 1-3 Kangemi Allstars

Migori Youth 1-1 Kenya Police

Thika United 2-1 St Joseph Youth

Kibera Black Stars 1-1 Modern Coast Rangers

Shabana FC 1-2 Kisumu Allstars