Habari MsetoSiasa

Ushuru zaidi waja – Ruto

September 4th, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

SIKU mbili tu baada ya ushuru wa asilimia 16 wa VAT kwa mafuta kuanza kutekelezwa, Naibu Rais William Ruto jana alitangaza kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza ada za kila mwezi za NHIF kwa wafanyakazi.

Akiongea katika Kaunti ya Kajiado, Bw Ruto alisema Serikali inapanga kufanyia marekebisho ada hizo ili wanaolipwa mishahara ya juu watozwe zaidi na hivyo kugharamia mahitaji ya watu maskini ambao hawana uwezo wa kujilipia ada hizo za kila mwezi

Alisema Sh1,700 zinazotozwa wafanyakazi wengi kila mwezi ni kidogo sana. “Tunapanga kubadilisha ada za NHIF ili wanaopata mishahara ya juu walipe zaidi,” akasema Bw Ruto.

Hatua hii ya Serikali itaongeza mzigo zaidi kwa Wakenya ambao wanaendelea kulimbikiziwa aina nyingi za ushuru. Mbali na nyongeza ya mafuta, majuzi gharama ya umeme ilipanda.

Naibu Rais alitangaza hayo huku athari za ushuru wa juu wa mafuta zikianza kudhihirika jana mamia ya wananchi walipoteseka kwa kutozwa nauli za juu na wengine kulazimika kutembea.

Mjini Mombasa, wamiliki wa matatu na waendeshaji bodaboda waligoma na kuondoa magari yao barabarani, huku wakazi wa Nakuru na Narok wakiandamana kupinga nyongeza ya bei ya mafuta kwa asilimia 16 kuanzia Jumamosi.

Wasafirishaji wa mafuta mjini Nairobi nao waligoma kulalamikia nyongeza hiyo.

Jijini Nairobi, wakazi wengi walikumbana na nyongeza ya nauli ya kati ya Sh10 na Sh100.

Wahudumu waliozungumza na Taifa Leo walisema walilazimika kupitisha kwa raia mzigo wa ushuru huo wa VAT, baada ya bei ya mafuta kupanda pakubwa na hivyo kuongeza kiwango cha matumizi ya mafuta.

“Kama hapa huwa tunalipisha Sh30 wakati wateja ni wachache na Sh60 asubuhi na jioni. Lakini sasa tumepandisha nauli hiyo kwa Sh10. Gari lilikuwa likitumia mafuta ya Sh5,000 kwa siku lakini sasa linatumia Sh6,500,” akasema mhudumu wa gari la kwenda mtaa wa Wangige.

Maeneo yaliyoathirika jijini ni pamoja na Thika, Juja, Kahawa West, Kasarani, Uthiru, Banana, Kangemi, Limuru, Juja na mengine mengi.

Kupanda kwa nauli kuliathiri pia wasafiri wa maeneo ya mbali huku wasafiri wa kuelekea Nakuru, Eldoret na Kisumu wakilipishwa Sh500, Sh1000 na Sh1,200 mtawalia.

Wahudumu walisema wateja wengi hawakupokea vyema ujumbe wa kupanda kwa nauli, wakisema wengine walisusia huduma.

Katika Kaunti ya Mombasa, mamia ya wasafiri wakiwemo wanafunzi walihangaika katika vituo tofauti vya magari ya usafiri, baada ya baadhi ya wamiliki wa magari ya usafiri wa umma kugoma kutoa huduma wakisusia ushuru mpya wa mafuta.

Baadhi ya wasafiri waliamua kutembea kwa miguu kwa safari za hadi kilomita tatu, huku wengine wakiamua kutumia magari ya Tuktuk na pikipiki kwa usafiri. Maeneo yaliyoathirika ni Mtwapa, Bamburi, Likoni na Jomvu.

“Kufikia saa moja na nusu asubuhi, hakukuwa na magari yoyote ya usafiri wa umma barabarani, saa moja baadaye machache yalianza kufika na kulipisha Sh100 hadi Jijini Mombasa ambapo huwa tunalipa Sh60 ndipo tukakataa kupanda. Baadaye walishusha nauli hadi Sh80,” akasema Bw Philip Kang’ethe.

Baadhi ya kampuni za mabasi pia zilitangaza kuwa zitaanza kupandisha nauli kuanzia wiki ijayo, baada ya gharama kupanda zaidi, hivyo zikiwataka wateja wao kujipanga kulipa zaidi.

Nyingi za kampuni za mabasi Mombasa na Nairobi hazikuwa zimepandisha nauli kwa wateja wao jana.

Mjini Nakuru, mwanasiasa Abdul Noor aliongoza wenye matatu na wakazi kuikashifu serikali

Mwenyekiti huyo wa zamani wa chama cha Jubilee tawi la Nakuru, aliitaka serikali itafute mbinu nyingine za kujipatia mapato ya ziada bila kumkamua mwananchi.

Meneja wa kampuni ya usafiri ya Mololine, Bw David Kahiga alisema haiwezekani kwa wahudumu wa magari ya usafiri wa umma kuendelea na biashara katika mazingira ya sasa bila ya kuongeza nauli.

Ripoti za DPPS, PETER MBURU, WINNIE ATIENO na JOSEPH OPENDA