Usicheze na Rais – Jenerali

Usicheze na Rais – Jenerali

Na COLLINS OMULO

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Jiji la Nairobi (NMS), Meja Jenerali Mohamed Badi amewaonya mahasimu wa kisiasa wa Rais Uhuru Kenyatta akisema kiongozi huyo wa taifa ana watetezi wenye ujasiri nyuma yake.

Jumatano ilikuwa mara ya kwanza kwa Badi kujitosa kwenye mijadala motomoto ya kisiasa inayoendelea nchini tangu ateuliwe na Rais Kenyatta kuongoza NMS mnamo Machi 2020.

Kwa muda mrefu sasa, baadhi ya viongozi katika Chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Kenyatta wametofautiana naye kuhusu masuala mengi ya uongozi.

Wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto, wanasiasa hao katika kikundi cha Tangatanga wamekuwa wakipuuza wito wa Rais kukomesha kampeni za mapema kuhusu uchaguzi wa 2022, na kuunga mkono mapendekezo ya kubadilisha katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Ni misimamo aina hii ambayo imefanya wadadisi wa kisiasa na hata baadhi ya wanasiasa na wananchi kwa jumla kuhisi kama kwamba, Rais Kenyatta amebaki mpweke, bila nguvu za kuwaadhibu wanaohujumu utendakazi wa serikali yake anapoelekea kustaafu urais mwaka ujao.

Jumatano, Jenerali Badi alifahamisha wanaoshikilia dhana kama hizi kuwa Rais ana kikosi kikubwa nyuma yake ambacho kiko tayari kulinda maazimio yake.

“Mimi si mwanasiasa kwa hivyo sitazungumzia BBI lakini hebu niseme wazi kwamba, Rais hayuko peke yake. Kama kuna handisheki, mbona mnafikiria yuko peke yake? Yuko pamoja na mshirika wake katika makubaliano (Raila). Mkisema yuko peke yake, kwani sisi tuko wapi? Rais ana Wakenya wote nyuma yake na sote ni watetezi wake,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika hafla ya kutoa cheki za mamilioni ya pesa kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu Nairobi. Mkuu huyo wa NMS aliamua kufungua roho baada ya masuala hayo kuhusu jinsi Rais alivyoachwa mpweke, kuibuliwa na Mbunge wa Kibra Imran Okoth.

Kulingana na Bw Okoth, Dkt Ruto amezama kwenye kampeni za mapema za urais 2022 na matokeo yake ni ukosefu wa nafasi ya serikali kutimizia wananchi ahadi za maendeleo zilizotolewa kabla uchaguzi uliopita.

“Kenya inapitia hali ngumu sana kwa sasa kwa sababu Rais ameachwa peke yake kutekeleza ahadi walizotoa 2017. Inasikitisha mno msaidizi wako anapokataa kukusaidia na badala yake anazunguka kila mahali akiendesha kampeni,” akasema Bw Okoth.

Mbunge wa Kibra alimkosoa Naibu wa Rais Ruto kwa kutumia rasilimali za umma kufanya kampeni kwa masilahi ya kibinafsi.

“Unatumia magari yaliyonunuliwa kwa fedha za walipa ushuru, unaishi kwenye nyumba iliyojengwa na Wakenya ilhali unatumia muda mwingi kukosoa serikali na kuhimiza Wakenya kukuchagua.

“Yamkini Naibu wa Rais aligundua tu hivi karibuni kuwa kuna mama mboga na wahudumu wa bodaboda nchini ilhali amekuwa serikalini kwa muda mrefu,” akaongezea.

Waziri Msaidizi wa Jinsia, Rachel Shebesh aliwashutumu wanasiasa ambao wamekuwa wakidai Rais Kenyatta hajafanya chochote huku akisema kuwa miradi iliyotekelezwa na serikali ya Jubilee inaonekana kila mahali.

Bi Shebesh aliwataka Wakenya kupuuzilia mbali madai yanayoenezwa na mahasimu wa Rais Kenyatta kuwa hajafanya lolote.

“Rais Kenyatta hafai kutangaza miradi ambayo ametekeleza kwani amefanya mengi. Kinachohitajika ni heshima. Siasa za 2022 zitakapowadia tutajitosa ulingoni lakini kwa sasa tuchape kazi,” akasema Bi Shebesh.

Viongozi hao pia walisema aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko alikwamisha miradi mingi ya maendeleo kwa kujihusisha na mizozo ya mara kwa mara.

You can share this post!

Man-City yaweka hai matumaini ya kutwaa mataji manne baada...

Sevilla wapepeta Barcelona kwenye mkondo wa kwanza wa...