Maoni

Usimcheke asiyejua Kiingereza kwa sababu si mizani ya werevu

Na DOUGLAS MUTUA August 9th, 2024 4 min read

WAKENYA si watu wazuri. Ngoja niseme sahihi zaidi: Wakenya ni waja wanoko waliojaa maudhi. Na katika maudhi yao, wakati mwingine wanashindwa kutumia akili.

Hivi imekuwaje tukawa tunawacheka watu wanaozungumza Kiingereza chenye makosa kana kwamba ndiyo lugha yetu ya mama? Mbona hatuwacheki na kuwadhulumu mtandaoni wanaokibeza na kukivuruga Kiswahili chetu kwa raha zao?

Hivi majuzi nusra Wakenya wamtimue kutoka mtandaoni msanii nyota wa Tanzania, Naseeb Abdul Juma Issack, anayedendwa na mashabiki wake ‘Diamond Platinumz’.

Kisa na maana? Amezungumza Kiingereza chenye makosa alipozuru Amerika kufanya ubia wa kikazi na msanii wa nchi hiyo, Jason Derulo.

Kauli iliyomletea fedheha Diamond ilitokea wakati wa mazungumzo yake na Derulo alipopokelewa kwenye uwanja wa ndege.

Derulo alipomuuliza aliwasili saa ngapi, Diamond alisema ‘pili’ badala ya ‘saa nane’.

Wakenya walichukua kauli hiyo wakakimbia nayo mtandaoni kumdhihaki jirani yetu huyo ambaye nyimbo zake – na hiki ni kinaya kabisa – ndizo maarufu zaidi nchini Kenya!

Tunamzungumzia Diamond, simba wa burudani Afrika Mashariki ambaye akikohoa tu, sijasema kunguruma, wasanii wote wa Kenya wanatahayari na kukunja mikia.

Tunamzungumzia Diamond, sogora wa kuunda fedha kisanaa, ambaye, nchini Kenya, huzoa malipo bora zaidi kutokana na umaarufu wa nyimbo zake kuliko wasanii wetu wote kwa sababu ndiye anayetamba redioni Kenya.

Tunamzungumzia Diamond ambaye, japo Wakenya tunajiambia eti tunazungumza Kiingereza safi kumzidi – baadhi ya wasanii wetu wasiojua hata maneno matatu ya Kiswahili kwa kuwa miaka yao yote hutumia Kiingereza – hawezi hata kufanya ubia wa kikazi nao.

Wasanii wa Kenya hawatoshi mboga. Hawaumi kitu mbele ya Diamond. Hata waliokwenda shule wakasoma shahada za uzamifu hawana lao, hivyo ‘Baba Dangote’ (Diamond) hawajui wala hawatambui.

Wengi wanatia dua kimoyomoyo kwamba iche siku moja awaite waimbe angaa wimbo mmoja naye ili wapate kujulikana. Hapo ndipo watakapojaribisha Kiswahili cha kila aina ili wakubalike kwake.

Mbele ya Diamond, hasa tunapozungumzia weledi wa kikazi na ukwasi wa kimapato, dharau na kero za Wakenya zitakuwa zimekwisha kwa kuwa, wasemavyo Wakamba, ujanja wa nyani huishia jangwani.

Acha pupa ya kulinganisha Kiingereza cha Derulo na Kiswahili cha Diamond, eti useme hata Derulo hajui Kiswahili; linganisha ufasaha wa Kiingereza cha vilimilimi Wakenya wanaomkejeli Diamond na ufasaha wa Diamond mwenyewe katika kunena Kiswahili.

Naseeb atajieleza kwa njia bora zaidi kokote kunakozungumzwa Kiswahili, akihitaji mkalimani ughaibuni apate, awaache ‘waingereza’ hao wa kupanga wakipaliwa na mate kwa ugumu wa kujaribisha Kiingereza chao ugenini! Wakiambiwa wako radhi kutumia Kiswahili, watamgeukia Diamond kwa sababu chake kipo, si kama chao cha kuombea maji, tena hakimpi mkalimani wa Kiingereza maumivu ya kichwa.

Kwa viwango vya waliobobea katika lugha hii tamu ya Kiswahili, Diamond hawi mnenaji bora wa Kiswahili Afrika Mashariki, lakini hajashuka hadi kiwango cha kukosolewa na Wakenya wanaomdhihaki. Wakatoe boriti zilizo machoni mwao kabla ya kuona kibanzi jichoni mwake.

Tunaokienzi Kiswahili tunajua jukumu muhimu analotekeleza Diamond katika makuzi ya lugha hii. Kwa nyimbo zake burudishi anakieneza kote duniani; baadhi yetu tunaungamana kwamba tumewahi kuzitumia kufundishia Kiswahili ughaibuni.

Isipokuwa Nyota Ndogo (Mwanaisha Abdalla) ambaye akitumia Kiswahili ipasavyo alipowika enzi zile, hakuna msanii Mkenya ambaye nimewahi kuwatajia wanafunzi wangu! Niwatajie nini? Sheng lugha ya wahuni? Tuheshimiane b’ana!

Aibu iliyoje kwamba wanaomcheka Diamond hawazidishi wala kupunguza chochote katika maisha yake.

Msanii Derulo, ambaye labda washamba wangetarajia aungane nao kumcheka Diamond na kujifanya hakuelewa alichomaanisha aliposema ‘pili’, hakuona ajabu.

Diamond alipofanya kosa hilo, Derulo alitumia akili zake razini, mantiki na muktadha akaelewa mara moja alichokusudia kusema, akampokea mgeni wake na kuendelea na ratiba yao kana kwamba hakuna kilichotokea.

Kando na kuelewa kwamba Kiingereza si lugha ya Diamond, Derulo alionyesha ukomavu wa akili na werevu wa hali ya juu ambao, kwa bahati mbaya, Wakenya waliotegukwa na mbavu wakimcheka jirani yao hawakuwa nao.

Kiingereza, au lugha yoyote ile, si mizani ya kupimia werevu wa mtu. Wataalamu wa lugha watakwambia kuwa lugha ni kama tabia anayojifunza mtu akaizoea, hivyo haipaswi kutumiwa kumdhalilisha yeyote.

Sasa utaringiaje watu na lugha ambayo – sawa na anayeigiza matege na akatembea kana kwamba alizaliwa nayo – umejifunza tu?

Sikatai, wanaokienzi Kiingereza watakwambia kuwa ndiyo lugha ya biashara duniani.

Hata hivyo, kauli hiyo si sahihi kikamilifu kwani sijawahi kusikia Wachina, ambao wanakwenda na Kichina chao kila pembe ya dunia, wameshindwa kutekeleza miamala ya kibiashara kwa kuwa Kichina kimekwama. Kwa taarifa yako, Kichina ndiyo lugha kubwa zaidi duniani.

Naandika haya kwa maana nina hakika waliomcheka Diamond ni wapuuzi wanaokidharau Kiswahili; kwetu Afrika mashariki ukizungumza Kiswahili kwa ufasaha inaaminika hukijui Kiingereza. Naam, hata ukiwa mwekezaji wa kupigiwa mfano, tena mlezi wa vipaji, kama Diamond.

Sawa na juhudi zinazofanywa kote duniani kuhifadhi turathi za kitaifa, binadamu anapaswa kujituma kudumisha milele lugha zote zinazozungumzwa kokote kule. Huo ni utajiri wa dunia.

Niite mfia lugha tukufu ya Kiswahili, ambayo kwayo Mwenyezi Mungu amenilisha na kunivisha, ila niachie Kikamba, Kikikuyu na lugha nyingine ndogo ninazozungumza kwa ufasaha.

Sitaki vizazi vijavyo visome kwenye vitabu vya kumbukumbu kwamba kulikuwa na lugha hizo ila hazisemwi tena na yeyote kwa sababu watu walitukuza Kiingereza au Kiswahili zaidi.

Tunapoanza kudharau lugha yoyote ile, hasa iliyo kubwa kama Kiswahili, basi tunaruhusu zile tunazoita za mama ziangamizwe, sote tuzungumze lugha moja.

Shughuli hiyo ya kuhujumu na kuangamiza lugha ndogo ikikamilika, mashairi yenye mnato na ngano tamu za lugha hizo zitaangamia pia, hivyo dunia itakumbwa na umaskini wa fasihi.

Sitaki wanangu waishi dunia ya aina hiyo. Natamani kila lugha idumu, tafsiri za sanaa zifanywe, kila jamii ifaidi kinachonogesha maisha ya jamii nyinginezo, hatimaye tuwe na ukuruba wa kitamaduni kote duniani.

Lugha za watu zingepuuzwa, ningekosa uhondo wa tafsiri za mashairi ya Anna Akhmatova, mshairi wa Urusi aliyebobea si haba. Wala wapenzi wa fasihi hatungemsoma Nikolai Gogol, mwandishi wa asili ya Ukraine aliyeandika tamthilia ya Mkaguzi wa Serikali.

Enzi ambapo ungemcheka mtu kwa kuzungumza lugha yake ya mama ilipitwa na wakati, sote tunapaswa kujivunia lugha zetu kwa kuwa ndio utambulisho wetu unaotupa upekee duniani. Tukijifunza za watu, basi tutakuwa wananchi wa kimataifa, wakwasi wa tamaduni.

[email protected]