HabariSiasa

Usipake Mzee Moi tope lako la ufisadi, KANU yamuonya Waiguru

August 30th, 2018 1 min read

WYCLIFFE MUIA na PETER MBURU

CHAMA cha KANU kimemkemea vikali gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru kwa kujaribu kumpaka Rais Mustaafu Daniel Moi tope la ufisadi katika kile walichokitaja kuwa ‘wizi wake wa kihistoria’.

Katika mahojiano na mwanahabari Jeff Koinange Jumatano usiku, Bi Waiguru alikosoa matokeo ya utafiti wa hivi majuzi wa kampuni ya Ipsos ambao ulimworodhesha kuwa wapili kati ya viongozi wafisadi zaidi nchini.

Alisema “Utafiti huo aidha uliniorodhesha juu ya Rais Mustaafu Moi ambaye aliongoza taifa hili kwa miaka 24… kwani unaweza kuwa wa upuzi namna gani? Kila mtu anafahamu kile tunadhani kuhusu enzi ya Moi. Unataka kusema niliiba zaidi ya Moi?”

Maneno yake hata hivyo hayajapokelewa vyema na chama hicho, ambacho sasa kimemwambia abebe msalaba wake mwenyewe bila kumhusisha rais huyo wa zamani.

“Gavana Anne Waiguru alisongoza wizi wa kihistoria katika shirika la NYS. Si vyema kuwa alimvuta Rais mustaafu Moi katika hali yake. Gavana abebe msalaba wake,” chama cha Kanu kikachapisha kwenye Twitter Alhamisi.

Katika mahojiano hayo, Gavana Waiguru alipuuzilia utafiti huo akisema ulilipiwa na maadui wake wa kisiasa.

“Ningependa kuelewa namna hiyo inapimwa: inapimwa kwa kuangalia kiwango cha pesa ambacho nimeiba? Nani ana ushahidi kuhusu pesa nilizoiba,” Bi Waiguru akauliza.

“Kwanini bado niko hapa badala ya katika mahakama ikiwa nimeiba hata senti moja kutoka kwa serikali?”