Habari

Usisikize uvumi kunihusu, Nyoro sasa asihi Uhuru

August 3rd, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro sasa amemhakikishia Rais Uhuru Kenyatta kwamba anaunga mkono serikali yake na Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Bw Nyoro pia alimtaka Rais Kenyatta kupuuzilia mbali uvumi kwamba hampendi na hamuungi mkono.

Bw Nyoro alitoa hakikisho hilo kwa dadake Bw Kenyatta, Bi Kristina Pratt, akimtaka kumfikishia Rais ujumbe huo.

Mbunge huyo amekuwa mshirika wa karibu wa Naibu Rais William Ruto na mwanachama wa kundi la ‘Tanga Tanga.’ Kundi hilo limeonekana kumkasirisha Rais Kenyatta kwa kuendeleza kampeni za 2022.

Bi Pratt, ambaye ni mwenyekiti wa Hazina ya Kitaifa ya Walemavu (NFDK) alikuwa akihutubu kwenye hafla ya ufunguzi wa ukumbi mpya wa maakuli katika Shule ya Walemavu ya Don Orione katika eneobunge hilo.

Bw Nyoro alipata nafasi ya kutoa ujumbe huo alipoamka kuhutubu. Uhusiano wa wawili hao haujakuwa mzuri.

“Wakati mwingine huwa tunaongea sana kwa kuwa sisi ni vijana. Hata hivyo, mwambie mimi ni mmoja wa marafiki wake wa karibu. Kila ninapopata nafasi, huwa ninawaambia watu kuhusu maendeleo aliyofanya. Tunampenda. Mwambie atutembelee ikiwa atapata nafasi,” akarai Bw Nyoro.

Kando na hayo, alieleza miradi ambayo imetekelezwa na Rais, akisisitiza kuwa ataendelea kumshukuru kutokana na ajenda za maendeleo ambazo ameanzisha katika kaunti hiyo.

Na katika kile kilionekana kuwa ujumbe fiche wa kisiasa, Bi Pratt alimshukuru Bw Nyoro, kwa kutambua kazi iliyofanywa na Rais Kenyatta, huku akiahidi kuwasilisha ujumbe wake.

“Ahsante kwa kutambua kazi ambayo Rais ameifanyia nchi. Nitamshukuru Rais kwa niaba yako na kumwasilishia ujumbe wako,” akaongeza.

Bw Nyoro amekuwa akisisitiza kuwa anamuunga mkono Rais kikamilifu, lakini baadhi ya viongozi wamekuwa wakimpelekea uvumi kwamba anapinga uongozi wake. Ametoa changamoto kwao kutoa video yoyote inayoonyesha akimkosea heshima Rais Kenyatta.

“Nunaunga mkono mikakati ya maendeleo inayoendeshwa na Rais. Hata hivyo, huwa nahisi vibaya wakati baadhi ya viongozi wanaeneza uvumi wa uongo watoto wa watu maskini wanapopata umaarufu kisiasa. Huwa wanasema kuwa tunampinga Rais Kenyatta. Ninawaambia kutoa ushahidi wowote. Ikiwa itathibitishwa, basi nitajiuzulu,” akasema Bw Nyoro.

Ajenda za maendeleo

Tayari, Rais Kenyatta amelikosoa kundi la Tangatanga hadharani mara kadhaa, akililaumu kwa kutozingatia ajenda nne kuu za maendeleo.

Uhusiano wao umekuwa mbaya kiasi kwamba kila wakati Bw Nyoro huanza kuhutubu, Rais Kenyatta huwa anaondoka na kurejea anapomaliza kuhutubu.

Mwaka 2018, Rais aliondoka kwa muda kwenye mazishi ya Bw Stanley Matiba wakati Bw Nyoro alipoanza kuhutubu.

Rais pia aliondoka wakati Bw Nyoro alipoanza kuhutubu kwenye mazishi ya mfanyabiashara Kamau Thayu.

Ujumbe wa Bw Nyoro unajiri wakati Rais Kenyatta anaonekana kuongeza juhudi zake kwenye vita dhidi ya ufisadi.

Wiki iliyopita, mbunge huyo alidai kuhusu ‘njama’ za kumfungulia mashtaka ya ufisadi.

Alisema kuwa njama hizo zinaendeshwa na mahasimu wake kwa kutangaza kwamba anamuunga mkono Dkt Ruto.