Habari za Kitaifa

Usitie saini mswada wa Fedha, 2024 – Maaskofu waambia Ruto


MAASKOFU wa Kanisa Katoliki Nchini wamemhimiza Rais William Ruto kutotia saini Mswada wa Fedha wa 2024 ili kutoa nafasi zaidi kwa ushirikishwaji wa maoni na mapendekezo kutoka kwa umma.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu hao (KCCB), Askofu Mkuu Maurice Muhatia, maaskofu hao Jumanne walisema maandamano ya Wakenya kupinga mswada huo yanaonyesha kuwa hawakubaliani na mapendekezo yake.

“Kufuatia fujo zilizoshuhudiwa jijini Nairobi na maeneo mengine nchini, Rais William Ruto hafai kutia saini mswada huu tata wa Fedha kuwa sheria. Serikali itoe muda zaidi kwa Wakenya kutoa maoni yao kwa mswada huo kwa lengo la kurejesha utulivu nchini,” akasema kwenye kikao na wanahabari katika afisi za KCCB mtaani Karen, Nairobi.

Askofu Muhatia alikashifu maafisa wa polisi na baadhi ya waandamanaji waliosababisha fujo zilizochangia maafa, majeruhi na uharibifu wa mali wakati wa maandamano hayo yaliyoshuhudiwa katika kaunti 27 nchini.

“Kwa mara nyingine tunaomba maafisa wa polisi kukoma kutumia nguvu kupita kiasi na hata kupiga risasi waandamanaji. Nao waandamanaji, wadumishe amani wanapotekeleza haki yao Kikatiba,” akaeleza.

Maaskofu hao pia waliwataka waumini wa Kanisa Katoliki kote nchini kuombea taifa la Kenya wakati wa kipindi cha siku tisa (90) cha Maombi ya Novena of the Sacret Heart of Jesus.

Awali, maandamano yalishamiri jijini katika barabara kadha za Nairobi wakati ambapo wabunge walikuwa wakishughulikia mswada huo kwa awamu ya tatu.

Hatimaye katika kura iliyopigwa wabunge 195 walifaulishw kupitishwa kwa Mswada huo huku wenzao 106 wakipinga.

Hatua hiyo ilikasirisha zaidi waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana barobaro maarufu kama Gen-Z, kiasi cha kuvamia majengo ya bunge na kuharibu mali.

Polisi walijibu kwa kutumia risasi dhidi ya waandamanaji hao na kuua idadi ya watu isiyojulikana.