Habari MsetoSiasa

USITUSAHAU: Wasioamini uwepo wa Mungu sasa wamlilia Ruto awachangie

September 10th, 2019 1 min read

NICHOLAS KOMU na AGGREY OMBOKI

CHAMA cha Wanaomkana Mungu (AIK) kimemuomba Naibu Rais William Ruto kuwakumbuka wao pia katika michango yake ya mara kwa mara kwa makanisa.

Katika hatua ya kinaya, wanachama hao wamemualika Dkt Ruto kuhudhuria mkutano wao wikendi hii huku wakimrai atoe donge nono kuwasaidia kuendesha shughuli zao nchini.

Dkt Ruto amekariri kwamba yeye ni Mkristo shadidi na kwamba, yuko tayari kutoa usaidizi wa kifedha kwa makundi yoyote ya kidini nchini.

Tangu yeye na Rais Uhuru Kenyatta wachaguliwe kwa awamu ya pili 2017, Dkt Ruto hutumia muda mwingi katika mikutano ya harambee makanisani ambako ametoa michango ya zaidi ya Sh200 milioni.

Ni ukarimu huu ambao Rais wa AIK Harrison Mumia wanataka kufurahia pia.

“Tangu kuchaguliwa tena 2017, Dkt Ruto amekuwa mkarimu sana kwa makanisa. Kama chama, tungependa kumualika Naibu Rais kuwa mgeni mheshimiwa katika mkutano wetu Septemba 14, 2019 katika hoteli ya Metro, Nairobi.

“Tunaomba atutolee mchango ili chama chetu kiwe na fedha za kutosha kuendesha shughuli zake. Tuko na mikutano kila mwezi na tungependa iwapo angehudhuria,” Bw Mumia alisema katika taarifa.

Kwa mtu ambaye amejihusisha sana na masuala ya kidini, itasubiriwa kuona iwapo Naibu Rais atakubali mwaliko wa chama hicho ambacho kinaamini hakuna Mungu.

Licha ya kusajiliwa, AIK imekumbwa na masaibu hususan kwa sababu ya idadi ndogo sana ya wanachama na matatizo ya kifedha ambayo yamesababisha migawanyiko miongoni mwa viongozi.

Kulingana na taarifa hiyo ya AIK iliyotumiwa vyombo vya habari, Naibu Rais ameombwa kukubali imani zingine na hivyo kujumuisha AIK katika michango yake.

“Tunajua Naibu Rais anafahamu kama taifa tuko na imani tofauti tofauti. Tunampa changamoto kujumuika na wasioamini Mungu kama anavyoingiliana na Wakristo na Waislamu,” Bw Mumia alieleza.