Michezo

USIU-A yaifunza Sailors jinsi ya kucheza magongo

December 10th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MATUMAINI ya Sailors kumaliza sita katika jedwali la Ligi Kuu ya magongo ya wanaume yalimea mabawa ilipolimwa mabao 5-2 na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU-A Uwanjani City Park, Nairobi.

USIU-A ya kocha, Willis Okeyo ilifanya kweli licha ya kupokea upinzani mkali mbele ya wapinzani wao. USIU-A ilivuna alama zote kutokana na magoli ya Brian Kiplimo, Richard Wandera, Lawrence Makacha, Chidi Victor na Smith Ngari waliocheka na wavu mara moja kila mmoja.

Nao Abraham Musee na Douglas Nyerere kila mmoja alitingia Sailors goli moja. Matokeo hayo yalifanya USIU-A kumaliza ya sita kwa alama 26, tatu mbele ya Sailors.

Katika kipute cha Supa Ligi, Parkroad Badgers ambayo tayari imezoa tiketi ya kufuzu kushiriki Ligi Kuu muhula ujao, ilishindwa kufana na kutoka nguvu sawa mabao 2-2 na Kisumu Youngstars.

Kisumu ilifunga kupitia Philip Omunyinyi na Derrick Jabali nao Arnold Abedy na Moses Chebukati walitingia Parkroad Badgers.

”Bila shaka tunashukuru wenzangu kwa kujitahidi na kujiongezea alama moja baada ya kiasi kihimili makali ya wageni wetu,” nahodha wa Parkroad, Brian Mwangi alisema na kuongeza kuwa wanapania kukaa ngumu kwenye mechi mbili zilizosalia.

Nacho Chuo cha Multimedia (MMU) kilikomoa Chuo cha Kenyatta (KU) 2-0, Impala ilipondwa 2-1 na Mombasa Sports Club huku Chuo cha Mt Kenya (MKU) na Chuo cha Nairobi (UoN) zikiagana sare tasa.