Michezo

USIU-A yapata matokeo mseto katika ligi ya hoki

September 24th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU za wanaume na wanawake za mpira wa magongo za Chuo Kikuu cha USIU-A, ziliandikisha matokeo mseto kwenye Ligi Kuu, Jumapili.

Wanaume wa USIU-A walishangaza Greensharks kwa bao 1-0 nao wanawake almaarufu Spartans wakalemewa 2-1 na Amira Sailors uwanjani City Park jijini Nairobi.

Timu ya wanaume ya USIU-A, ambayo inanolewa na kocha Willis Otieno, ilipata mtihani mgumu mbele ya mabingwa wa zamani Greensharks.

Pande zote zilionyesha mchezo wa kusisimua kabla ya USIU-A kufanikiwa kuzamisha Greensharks kupitia bao la Lawrence Makacha na kupiga hatua moja kwenye jedwali. “Nashukuru wachezaji wangu kwa kujitahidi na kulemea wapinzani wetu maana kusema kweli mechi haikuwa rahisi,” alisema Otieno.

Spartans ilipoteza pointi zote na kushuka hatua moja baada ya kuzabwa na Amira Sailors kupitia mabao ya Leah Omwadho.

Veronica Maua alifungia USIU-A bao la kufuta machozi.

Spartans ilizidiwa maarifa na wapinzani wao licha ya kuonyesha dalili za kuamka baada ya kutandika Silders 1-0 wiki moja iliyopita.

Kufuatia matokeo hayo, Butali Warriors inaongoza Ligi Kuu ya wanaume kwa alama 30 kutokana na mechi 12.

Malkia wa mchezo huo Telkom wamekalia juu ya Ligi Kuu ya wanawake kwa alama 26, nane mbele ya Scorpions ya Chuo Kikuu cha Strathmore.