Michezo

USM Alger walalamikia jua kali kwenye mechi dhidi ya Gor Mahia

August 27th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

Mashabiki wa timu ya USM Alger nchini Algeria wamelalamikia mechi yao dhidi ya Gor Mahia hapo Agosti 29, 2018 kusakatwa saa nane mchana, saa za Algeria (saa kumi jioni saa ya Kenya).

Wakizungumzia mechi hiyo ya marudiano ya Kombe la Mashirikisho la Afrika ya Kundi D, wamekasirishwa na saa hiyo, ambayo hupangwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), wakidai kwamba jua litakuwa kali sana wakati huo.

Shabiki Nozha Driss aliuliza, “Kwa nini saa nane mchana? Nani alifanya uamuzi huu?”

Salah Bentalha, “Wakati huo jua litakuwa utosini na kali kwelikweli.”

Manil Sabeer, “Saa nane mchana!!!” Abdelaziz Ben Kabel amesema mchuano huo ulifaa kuchezwa wakati moja na ule unaokutanisha Rayon Sports (Rwanda) na Young Africans (Tanzania) jijini Kigali utakaoanza saa moja baada ya USM Alger na Gor kuteremka uwanjani.

Mashabiki wa Gor na USM Alger wamekuwa wakitaniana, kila mmoja akivutia kamba upande kwao, kambi zote zikijaa matumaini zitaibuka na ushindi.

Gor inaongoza kwa alama nane sawa na USM Alger, ambyo imefunga mabao machache. Rayon, ambayo ilizaba Gor 2-1 jijini Nairobi mnamo Agosti 19, inashikilia nafasi ya tatu kwa alama sita. Itamenyana na Young Africans, inayovuta mkia kwa alama nne. Mshindi kati ya Gor na USM Alger ataingia robo-fainali bila ya kutegemea matokeo ya mechi kati ya Rayon na Young Africans. Rayon itaaga mashindano ikitoka sare. Hata hivyo, itajikatia tiketi ya kushiriki robo-fainali ikishinda halafu mmoja kati ya Gor na USM Alger apigwe. Droo ya robo-fainali itafanywa Septemba 3, 2018.