USWAHILINI: Huu hapa mseto wa milo inayopendwa mno katika janibu za Uswahilini

USWAHILINI: Huu hapa mseto wa milo inayopendwa mno katika janibu za Uswahilini

Na HAWA ALI

BAADHI ya vyakula maarufu vya Waswahili vinavyopikwa kwa unga wa ngano ni pamoja na mandazi, mikate ya kusukuma/chapati, mikate ya upawa/magole/mikate ya maji, mahamri, makarara/kombo alawi, kaimati, vipopoo/vitobwesho, tambi, mikate ya ufuta, mikate ya mayai, ajemi, mikate ya maziwa, mikate ya kusuka, manda na mikate ya pau.

Pia vileja vya aina mbalimbali kwa ladha na maumbo tafauti tofauti.

Kwa kawaida kuna milo mikuu mitatu miongoni mwa jamii za Waswahili.

Mlo wa kwanza ni chakula cha asubuhi/chai/kifungua kinywa. Mlo huu aghalabu huwa ni kinywaji kama chai inayoandaliwa kwa kuchemsha maji na kutia majani ya chai, sukari na viungo kama hiliki na mchaichai kwa chai ya rangi na ikiongezwa maziwa huitwa chai ya maziwa.Chai hunywewa pamoja na kitafunwa kama chapati, maandazi/mahamri au vitumbua. Vitafunio hivi huandaliwa kwa ustadi mkubwa na huwa na ladha ya kupendeza. Ni maarufu pia kwa jamii ambazo si Waswahili.

Pili, ni mlo wa mchana (chamcha); mlo huu huwa na chakula kikuu kama wali wa nazi au ugali pamoja na kitoweo kama mchuzi wa kuku au samaki wa kukaanga pamoja na mboga mboga au viongeza ladha kama pilipili. Hiki ndicho chakula kinachothaminiwa zaidi kwa kuwa ndicho kinachompa mtu nguvu za kuendelea na shughuli za kutwa nzima.

Mlo wa mwisho ni chakula cha jioni (chajio); mlo huu mara nyingi hufanana na ule wa mchana, lakini baadhi ya watu hupendelea kula vitafunwa kama chapati au mikate kwa mlo wa jioni pia.

Mapishi

Kuna namna kadhaa za kuandaa vyakula kama vile kwa kuchemsha, aghalabu kuku au samaki mwanzo huchemshwa.

Kuna vyakula vya kukaangwa kwa mafuta kidogo aghalabu kuandaa mchuzi.

Namna nyingine ni kuoka; vyakula vya kuoka ni kama mkate. Zamani watu walitumia makaa kuoka vyakula vya aina hii lakini siku hizi wengi wamehamia katika uokaji kwa majiko ya umeme au gesi.

Vile vile, kuna vyakula vya kubanika. Hivi ni pamoja na samaki, mishikaki au nyama choma.

Mwisho ni vyakula vya kukaangwa kwa mafuta mengi; vyakula hivi ni kama vile mandazi au kuku wa kukaanga.

Kuna vyakula mahususi kwa ajili ya shughuli maalumu. Kwa mfano, chakula cha karamu katika shughuli kama vile harusi, aghalabu huwa pilau, biriani au wali mweupe kwa mchuzi wa kuku, nyama au hata samaki kutegemea na hali, mahali au mahitaji ya mtu.

Katika hafla ya harusi inayofanyika nyakati za jioni au usiku hasa sehemu za mijini, huandaliwa halua, sambusa, kababu, katlesi, keki, vileja, vitoweo kama vile nyama, ngisi, pweza, kuku au maini yaliyokaushwa au kukaangwa.

Sadaka ya halua, visheti, tende au biskuti hutolewa katika mikusanyiko ya kijamii kama vile ndoa, maulidi, khitma au hata maziko.

You can share this post!

Ripoti ya utafiti yachora taswira ya viwango vya umaskini...

NGILA: Serikali isianzishe mradi mpya, ikamilishe Konza