Makala

USWAHILINI: Matumizi kedekede ya udi miongoni mwa jamii za Waswahili

September 11th, 2019 2 min read

Na HAWA ALI

KWA wakazi wa jamii za Waswahili, manukato ya udi ni sehemu muhimu ya vitu vinavyokuwemo katika vijaluba vya vipodozi vyao.

Udi una manukato yanayokaa mwilini na kwenye nguo kwa muda mrefu, na kwa mujibu wa desturi za watu wa mwambao, udi unaaminiwa zaidi kuliko manukato mengine ya kisasa.

Udi ni mchanganyiko wa mti wenye riha, sukari na mafuta ya manukato na huwa ama kama vipande au unga unga. Ukiwekwa kwenye chetezo chenye mkaa uliowashwa na kuanza kufukizwa udi hutoa harufu ya waridi.

Udi unatumika kwa njia mbali mbali na katika matukio mbali mbali. Kutokana na imani za watu wa mwambao, vyumba vilivyofukizwa moshi wa udi haviwi tu na harufu ya waridi bali pia hukaribisha ruhani wazuri nyumbani.

Udi upo wa aina nyingi na hutumika kwa matumizi mbalimbali. Kuna udi wa njiti ambayo ni ya kuchoma na zipo aina tofauti na harufu tofauti, kuna udi wa kumimina kwenye maji kisha unayaogea na kadhalika.

Udi hutumika kufanya dua au maombi kulingana na imani ya mtu.

Mara nyingi hutumika majumbani au kwenye maduka.

Wengi wa wanawake wa mwambao hutumia udi katika makabati yao ya nguo na katika masanduku kama njia ya kuzipa manukato nguo zao.

Kuamsha hisia

Udi pia unatumiwa zaidi kama chambo au kivutio cha mapenzi kwa wanaume wa Pwani.

Ni aina ya kishawishi cha kuamsha ‘ashiki’ ya wanaume.

Kwa kawaida kila jioni baada ya kuoga wanawake wa mwambao hujifukiza udi bila kujikausha maji katika miili yao.

Ingawa kumekuwa na maendeleo ya teknolojia ya utengenezaji wa vyetezo vya umeme na ambavyo ni rahisi kwa kujifukiza, wanawake wengi wanapenda kutumia njia ya asili ya kujifukiza udi kwa kutumia mkaa

Udi hutumika sana wakati wa ndoa na sherehe nyingine za kidini. Ni kitu cha kawaida kwa bibi arusi na bwana arusi kutumia udi.

Kwa kawaida vazi la bibi arusi na nguo zake nyingine anazokwenda nazo kwa mumewe hufukiziwa udi.

Wanawake wengi hujifukiza zaidi udi wanapokuwa katika siku za mwezi ili kuondoa harufu mbaya ya damu ya mwezi.

Na ni sifa kubwa kwa mwanamke hukajifukiza udi ukolee na ukipita pahali basi ukaacha harufu ya udi hata kama hutoambiwa basi lazima hutapata sifa sana, mwanamke yule ananukia udi

Udi pia hufukizwa chumba kikanukia,nguo na mwili zikanukia pia. Mara nyingi wanawake wakiandaa nguo za waume zao hasa kanzu huzifukiza na udi. Na pia kuna mafuta ya udi ambayo siku hizi wengi hutumia.

Pwani udi ni kama chai kwenye sukari. Mwanamke hujifusha akanukia akamngoja bwana.