USWAHILINI: Mnara wa pembe jijini Mombasa ndio nembo kuu ya Uswahilini

USWAHILINI: Mnara wa pembe jijini Mombasa ndio nembo kuu ya Uswahilini

Na HAWA ALI

MNARA wa pembe za ndovu ndio alama kuu ya Uswahilini humu nchini.

Mnara huu unapatikana katika barabara kuu ya Moi-Kilindini katikati ya mji wa Mombasa.

Pembe hizi zinaashiria kuwa Pwani ya Kenya na hasa Mombasa ni chimbuko la kivutio kikubwa cha watalii Afrika Mashariki. Hili limewafanya wageni wengi kufika kwenye mnara huu na kukata kiu cha utalii wao. Ni mnara ulio na urefu wa takriban futi 60.

Yaelekea kwamba pembe hizi zilisimikwa katikati ya jiji la Mombasa ili kuwavutia watalii kutoka Afrika Mashariki , bara la Afrika na mataifa ya Ulaya. Pembe hizo zilitengenezwa kwa kutumia mabati maalumu ya chuma kisha yakawekwa barabarani zikiwa zimepishana kileleni ili yasitatize uchukuzi wa magari. Kihistoria watumwa waafrika walibebeshwa pembe za ndovu waliouawa ili kuwapelekea mabeberu wale.

Inadaiwa pia kwamba ndovu hizo zinamaanisha kuwa ndovu walikuwepo kwa wingi katika enzi ya utawala huo wa mkoloni katika mbuga ya Tsavo Magharibi na mbuga ya Mwalughanje eneo la Kinango na Shimba Hills huko Kwale.

Kwa hivyo pembe zilizoko kwenye barabara kuu ya Moi mjini Mombasa zina historia ndefu mbali na kuutangaza utalii wa pwani. Pia zinaashiria masaibu yaliyowapata waafrika waliobebeshwa pembe halisi za ndovu kutoka mbugani hadi kwenye mahema ya matajiri ufuoni mwa bahari hindi.

Enzi hizo Waafrika walionunuliwa na wazungu kutoka kwa Waarabu walifanyishwa kazi za sulubu. Waliochoka au kuugua walitumbukizwa baharini wafe au waliwe na samaki

Wahisani waliridhishwa na mbinu hiyo ya kuutangaza utalii ambao ni kivutio kikubwa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.

Picha inayojengwa na pembe hizo ni utamaduni wa Waswahili kwa wanaozuru Pwani na katika maeneo ya uswahilini kwa jumla.

You can share this post!

SAUTI YA MKEREKETWA: Pumzika kwa amani Jemedari Magufuli

VITUKO: Suala la chanjo kwa walimu lawa kiazi moto katika...