USWAHILINI: Turathi ya Misitu ya Kaya na manufaa yake kwa Wamijikenda

USWAHILINI: Turathi ya Misitu ya Kaya na manufaa yake kwa Wamijikenda

Na HAWA ALI

JAMII ya Wamijikenda ni kabila linalopatikana Pwani ya Kenya, na moja ya utambulisho wao ni Kaya – hii ni misitu ambako wanaishi, na ambayo huchukuliwa kuwa mahali patakatifu.

Utamaduni huu unajumuisha pia maadili na usimamizi wa jamii. Licha ya umuhimu wake, kudidimia kwa raslimali ya ardhi na ukuaji wa miji ni tishio kwa tamaduni ambazo zinaendana na Kaya, na hivyo kuhatarisha turathi hii ya jamii ya Wamijikenda.

Misitu katika eneo hili hutoa uhifadhi wa rasilimali na huduma nyingine kama malisho kwa mifugo malighafi kwa viwanda, uhifadhi wa maji, kulinda chemchemi za maji, ulinzi wa mazingira, kudhibiti mmomonyoko wa udongo na virutubisho vya ardhi.

Hata hivyo, mchango huu haujumuishi faida nyinginezo kama utoaji wa kuni na makaa, asali, thamani kwa mazingira na mazao mengine ya misitu.

Kunazo Kaya zaidi ya 52 katika wilaya za Kwale na Mombasa na 39 katika eneo la Kilifi. Mingi ya misitu hii haijaangamizwa kabisa.

Neno “Kaya” linamaanisha maboma ama vijiji vidogo ambavyo vilitengenezwa na Wamijikenda na kwa mujibu wa historia, misitu hii ilihifadhiwa kuanzia mwanzo wa karne ya 16.

Wamijikenda hutumia misitu ya Kaya kufanya hafla na maadhimisho ya kijamii, kama maafa au kwa kuzika waliofariki; na vile vile ni pahali pa maombi na chanzo cha mazao kama vile matunda, dawa za kiasili na faida nyinginezo nyingi.

Mbali na umuhimu wa rasilimali ya misitu kwa uchumi wa taifa, zipo changamoto kadhaa zinazokabili maendeleo ya sekta hii.

Changamoto hizo ni pamoja na ukataji miti ovyo, kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi, kuni na ukosefu wa mipango kabambe ya kutumia rasilimali ya misitu ipasavyo.

Msitu wa Arabuko-Sokoke umeenea kilomita mraba 420 kuanzia Bahari ya Hindi wilayani Kilifi na kuenda hadi Malindi takribani kilomita 110 Kaskazini ya Mombasa.

Ni mojawapo ya masalio ya kiasili nchini Kenya na ambayo ni makubwa zaidi ya msitu kamili katika pwani ya Afrika Mashariki.

Msitu huu hutoa hifadhi kwa wanyama wengi.

Misitu ya kaya kwa sasa inavamiwa na kukatwa kwa minajili ya kufanywa kuwa makazi ya watu, hatua ambayo ni kinyume cha mila za tamaduni za jamii ya Wamijikenda.

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Ken Walibora anavyoendeleza taswira ya...

VITUKO: Pengo atua kijijini na kutumwa na kanisa jijini...