UTACHEZA NA WATOTO! Koscielny kupewa adhabu ya kutisha

UTACHEZA NA WATOTO! Koscielny kupewa adhabu ya kutisha

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

LAURENT Koscielny atalazimishwa kufanya mazoezi na watoto kama adhabu ya mvutano kati yake na klabu ya Arsenal ambao mwenyewe anaamini usingeshuhudiwa iwapo Arsene Wenger angekuwa bado usukani.

Saa chache baada ya Arsenal kutangaza kuajiri beki chipukizi William Saliba, 18, kutoka Saint-Etienne na Dani Ceballos, 22, kutoka Real Madrid, vyombo vya habari nchini Uingereza vimesema kuwa Koscielny amekuwa akiambia wenzake katika uwanja wa kufanyia mazoezi wa London Colney kuwa tukio hilo lisingewezekana chini ya Wenger.

Koscielny amekuwa akijaribu kulazimisha uhamisho wake baada ya kukosa kuelewana na Arsenal kuhusu kandarasi mpya na hata alikataa kujiunga na timu ilipokuwa ikifanya ziara ya kujiandaa kwa msimu mpya nchini Marekani.

Beki huyu amesalia na mwaka mmoja katika kandarasi yake ya mshahara wa Sh12.9 milioni kila wiki na alitumai kuiongeza, lakini hakufikia mapatano na Arsenal na kuamua kugoma.

Licha ya kuwa kikosi cha kwanza cha Arsenal kimerejea kutoka Marekani, Koscielny atalazimika kufanya mazoezi na watoto kwa sababu ya tabia yake. Anatarajiwa pia kupigwa faini na klabu kutokana na kitendo chake.

Arsenal ilitangaza kusajli Saliba kutoka Saint-Etienne mnamo Alhamisi kwa ada ya Sh3.4 bilioni, saa chache tu baada ya kufichua kuwa kiungo Ceballos amejiunga nayo kwa mkopo wa mwaka mzima kutoka Madrid.

Saliba hatachezea Arsenal msimu wa 2019-2020 baada ya kurejeshwa Saint-Etienne inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ufaransa kwa mkopo. Ataanza kuchezea Arsenal msimu 2020-2021.

Saliba alikuwa sajili wa pili kuthibitishwa na Arsenal ndani ya saa mbili.

Arsenal inaaminika ilikuwa imevutiwa na Saliba kwa muda mrefu. Kandarasi ya Ceballos ni ya msimu mmoja.

Kuisadia timu ya taifa

Mhispania huyu, ambaye alicheza mechi 23 za Ligi Kuu nchini humo msimu 2018-2019, alisaidia timu ya taifa ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21 kuibuka mabingwa wa Bara Ulaya mnamo Juni 2019.

“Tunafurahia sana kuona Dani amejiunga nasi,” alisema kocha wa Arsenal, Unai Emery. “Yeye ni mchezaji aliye na talanta ya hali ya juu, ni mbunifu na mzuri katika ukamilishaji wa pasi.”

Naye Ceballos alisema, “Kocha Emery alichangia pakubwa katika mimi kujiunga na klabu hii kubwa.

“Yeye ni Mhispania na ananifahamu kwa miaka mingi nikichezea klabu nyingine. Nafurahia sana kuja hapa kusaidia Arsenal kutimiza malengo yake.”

Aidha, Arsenal imeanzisha tena mazungumzo ya kutafuta huduma za Kieran Tierney kutoka Celtic.

Ripoti nchini Scotland zinasema kuwa Arsenal inataka sana kunyakua Tierney katika kipindi hiki cha uhamisho na inaaminika kuwa klabu hizi zinakaribia kuafikia makubaliano.

Ofa mbili za Arsenal zimekataliwa na Celtic, licha ya klabu hii kutoka jijini London kufikia bei ya Sh3.2 bilioni ambayo iliitishwa.

Inasemekana Celtic ilikataa ofa hiyo kwa sababu Arsenal ilitaka ilipe fedha hizo kidogo kidogo nayo ilitaka kiasi hicho mara moja.

You can share this post!

MAJONZI KWA SHUJAA: Mbunge Okoth aombolezwa

Pochettino aomba radhi baada ya farakano baina ya wachezaji...

adminleo