Kimataifa

UTAFITI: Inawachukua wakuu wa kampuni siku 1 kupata mshahara wako wa mwaka mzima

January 23rd, 2019 2 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

UTAFITI kuhusu mishahara kati ya waajiri na wafanyakazi wao katika mataifa 22 duniani umedhihirisha kuwa wasimamizi wengi wa kampuni mbali mbali hupokea mishahara ya juu Zaidi ikilinganishwa na wafanyakazi.

Katika ufichuzi wa kushangaza, baadhi ya Maafisa Wakuu Wasimamizi wa kampuni zinazofanya vyema hupokea mshahara mkubwa kushinda wafanyakazi wao, pesa wanazopokea baadhi yao kwa saa kadha tu kwa siku zikizidi mshahara wa wafanyakazi wao wa mwaka mzima.

Ili kurahisisha mambo, kufikia Januari 4 Januari, kunao maafisa wakuu watendaji wa kampuni Fulani ambao tayari walikuwa wamepokea pesa Zaidi ya mishahara ambayo wafanyakazi wao watapokea mwaka 2019 hadi mwisho.

Utafiti huu ulitekelezwa na kampuni ya Bloomberg, katika mataifa ya India na Marekani, tofauti za kimishahara kati ya wafanyakazi na waajiri zikiwa juu zaidi.

Utafiti ulibaini kutambua pesa zaidi ambazo maCEO wa kampuni tofauti hupokea ikilinganishwa na wafanyakazi wao.

Nchini US, utafiti huo ulionyesha kuwa maafisa hao hutumia chini ya siku mbili kupata mshahara ambao wafanyakazi wao hupokea kwa mwaka mzima.

Nako nchini India, maafisa hao hutumia hata muda mfupi Zaidi, utafiti ukionyesha kuwa kwa takriban roobo tatu ya siku, wanaweza kupokea mshahara sawa na wa wafanyakazi wao wa siku 365.

“Pengo la mshahara kati ya waajiri na wafanyakazi lilipanuka huko US ikilinganishwa kati ya 1980 na 2016,” mwandishi wa US Sam Pizzigati, mwandishi wa kitabu cha The Case for a Maximum Wage ambacho kilizinduliwa mwaka uliopita.

“Katika kampuni nyingi kubwa kubwa, mfanyakazi wa kawaida atatumia takriban miaka 30 ya kufanya kazi ili kufanikiwa kupata pesa anazopata Afisa Mkuu Mtendaji kwa mwaka mmoja tu. Katika kampuni ya McDonald’s, mfanyakazi wa kawaida atatumia miaka 3,101,” utafiti ukaonyesha.

Maafisa wa kutoka Uswizi nao wanahitaji takriban siku mbili tu kupata pesa anazopata mfanyakazi wa kawaida kwa mwaka mzima.

Hali hiyo inapobadilishwa kuwa mshahara wa wiki moja wa CEO, mataifa mengi Zaidi ya dunia yanajiunga katika mkondo huo wa maafisa wanaolipwa pesa nyingi Zaidi ikilinganishwa na wafanyakazi wa kawaida.

Nchini Afrika Kusini, CEO atahitaji siku tatu tu kupata mshahara wa mwaka mzima wa mfanyakazi wake wa kawaida, nako China siku 2.11.

Kampuni za US ndizo zinawalipa maafisa wake wasimamizi pesa nyingi Zaidi, ambapo CEO wa kawaida hulipwa Zaidi ya Sh1.4bilioni kwa mwaka.

Nchini Nigeria, CEO anayelipwa mshahara mkubwa zaidi, Austin Avuru wa kampuni ya Seplat Petroleum Development hupokea Sh1.3bilioni kwa mwaka. Kulingana na ripoti ya SalaryExplorer.com mapato ya kawaida huko Nigeria ni Sh1.6milioni kwa mwaka, ikionyesha kuwa afisa huyo anaweza kupokea pesa hizo kwa chini ya siku tano.

Nchini Russia nako mambo ni magumu Zaidi kwani mshahara wa mwaka wa maCEO 25 ulipotafitiwa mnamo 2016 ikilinganishwa na mshahara wa kawaida wa taifa hilo, ilionyesha kuwa maafisa hao wanatumia nusu ya siku kupata pesa anazopata mfanyakazi wa kawaida kwa mwaka mzima.

Nchini Brazil nako maafisa wa kawaida wanatumia siku nane tu kupata pesa anazopata mfanyakazi wa kawaida kwa mwaka.

Suala hili mara kwa mara limeibua kivutano katika sehemu tofauti za ulimwengu, umma na wakosoaji wakitaka kuelezewa sababu za kuwepo kwa tofauti kubwa kiasi hicho, kati ya mshahara wa maCEO na wafanyakazi wao.