Kimataifa

UTAFITI: Utanashati kazini humzimia mwanamume ndoto zake maishani

November 13th, 2018 2 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

JE, wewe ni mwanaume mtanashati? Ikiwa jibu lako ni ndiyo, na una ndoto ya kujikuza kazini basi una sababu ya kutia shaka, hii ni kwa kuwa utafiti wa vyuo vikuu viwili kutoka Uingereza na Marekani umebaini kuwa wanaume watanashati huenda wakadhulumiwa kazini na kukosa kutimiza ndoto zao za kujikuza, kwa kuonewa kijicho nan a mabosi, haswa wanaume wenzao.

Utafiti huo umebaini kuwa wanaume watanashati wana nafasi ndogo ya kupata kazi za ndoto zao, na kuwa wawapo kazini mabosi wa kiume huwaona kama tishio.

Hivyo, hali hii inawafanya kunyimwa nafasi za kufanya kazi ambazo zinaweza kuanika vipaji vyao, ili wasipate nafasi ya kujikuza, wakasema watafiti hao.

Badala yake, wanaume hawa huishia kupewa kazi zisizo na maana na ambazo ushindani wao wa kimaumbile hauonekani nje, japo watafiti walisema wanawake warembo hawakumbani na changamoto hii.

Utafiti huu ulifanywa kwa ushirikiano wa vyuo vikuu vya London’s School of Management na University of Maryland, US, baada ya visa vine halisi ofisini.

Ulibaini kuwa wakatoi wanaume wanawaajiri wanaume wenzao kufanya kazi pamoja, maumbile ya anayeajiriwa huwa sehemu ya kile kitakachoamua ikiwa atapewa kazi hiyo.

Lakini kinaya ni kuwa, kwa wanawake kuwa mrembo kunakuongezea nafasi ya kupata kazi kwa kuwa hali hiyo imechukuliwa kuwa ubora.

Mtafiti mkuu katika chuo kikuu cha Maryland Prof Sun Young Lee alisema kuwa “Mameneja huathiriwa na Imani zilizopo na huwa wanafanya maamuzi ya kuajiri wakizingatia mahitaji yao ili kampuni zisipate wafanyakazi walio na ushindani mkubwa kuwashinda.”

Kufuatia hali hii, watafiti hao walishauri kuwa mbinu za uajiri kuboreshwa Zaidi ili kuhakikisha kuwa watu wengine hawanyimwi nafasi za kazi kutokana na sababu za kibinafsi.

Utafiti huo unatarajiwa kuchapishwa katika jarida la Organizational Behavior and Human Decision Processes na umetolewa baada ya msanii Rob Lowe kulalamika mwaka uliopita namna wakati mmoja alishindwa kukuza taaluma yake kwani utanashati wake ulikuwa kikwazo.

Watafiti walisema kuwa kutokana na hayo, mwanamume mtanashati kupata cheo kazini ni kibarua na huenda akazeeka bila kutimiza ndoto yake.

Matokeo yake ni kuwa kuwa mtanashati Zaidi kunaweza kuadhiri taaluma ya mwanaume na kujikuza kikazi.

Sababu nyingine iliyotolewa ni hali ya mameneja kuzima ushindani wa kuunda uhusiano na wanadada warembo ambao wanaweza kuwa kazini.