Makala

Utafiti umegundua washukiwa wengi wa wizi na uhalifu huvalia jezi za Arsenal

April 23rd, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

UTAFITI umegundua washukiwa wengi wa wizi na uhalifu huwa wamevalia jezi za Arsenal.

Haya ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa nchini Malawi na John Hatman.

Sasa gumzo na cheche zimewaka mitandaoni nchini Kenya huku mashabiki wa Arsenal wakikerwa na mahasimu wao wa timu za Manchester United, Chelsea, Liverpool na wengine.

Ripoti hiyo ilitolewa ikiwa na anwani: “Jezi za Uhalifu: Uchunguzi wa Ushabiki wa Kandanda na Wizi nchini Malawi.”

“Utafiti huu unachunguza matukio yanayozidi Malawi ambapo washukiwa waliohusishwa na wizi, hata kuvunja nyumba za watu, mara nyingi hukamatwa wakiwa wamevalia jezi hususan zinazohusiana na timu ya Arsenal,” ulieleza utangulizi wa ripoti hiyo.

Uchunguzi huu umebaini Hatman alizamia upelelezi ili kung’amua kama ushabiki wa mpira wa miguu unahusiana na matukio ya uhalifu.

Mahabiki wa Arsenal wasingetaka mashabiki sugu wa Manchester United kama vile Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen waone ripoti hii.

Bw Murkomen hakuchelewa na akaanza kuwadhihaki mashabiki wa Arsenal kwenye mitandao ya kijamii.

“Wataalamu Malawi wanashughulika sana kutafiti matukio yanayozidi kuongezeka ambapo washukiwa wa wizi aghalabu huwa mashabiki wa Arsenal,” Bw Murkomen alipakia kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X kabla ya kuvamiwa na mashabiki wa Arsenal waliorejesha kejeli kwa Manchester United inayosuasua msimu huu.