Habari Mseto

Utahesabiwa utakapokuwa usiku wa Agosti 24 – Serikali

August 18th, 2019 1 min read

CHARLES WASONGA na WALTER MENYA

SERIKALI imesema hakuna haja ya watu wanaoishi mijini kusafiri mashambani kushiriki shughuli ya kuhesabu watu ikayoanza Jumamosi hii.

Mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), Zachary Mwangi aliwataka wananchi kupuuza wito wa wanasiasa wanaotaka wananchi warudi makwao wakahesabiwe Agosti 24.

“Ni muhimu kwa watu kuhesabiwa mahala wanapoishi. Kwa hivyo, tunawahimiza wanaoishi mijini kutosafiri mashambani kwani wakifanya hivyo, kaunti za mijini zitakosa mgao wa kutosha wa rasilimali,” Bw Mwangi akasema, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Wataalamu wa masuala ya kuchunguza takwimu husema ni muhimu takwimu zikusanywe bila kutatiza hali ya kawaida ya maisha, kwa hivyo inahitajika watu wawe wanaendeleza maisha yao kama kawaida wakati sensa ikifanywa.

Afisa huyo alifafanua kuwa takwimu kutokana na shughuli hiyo ya sensa zitatumika na Tume ya Ugavi wa Rasilimali (CRA) kugawia kaunti pesa.

Kulingana na mfumo unatumiwa sasa na CRA, asilimia 45 ya fedha zinazotengewa kaunti hugawanywa kwa misingi ya idadi ya watu.

“Kwa hivyo, kaunti zenye idadi kubwa ya watu zitapata kiwango cha juu cha rasilimali za kitaifa,” akasema Bw Mwangi.

Hii ndio imefanya wanasiasa wamekuwa wakiendesha kampeni za kuwahimiza wakazi wa mijini kusafiri maeneo ya mashambani ili kuhesabiwa huko.

Kwa mfano, Mbunge wa Mukurwe-ini, Anthony Kiai ameanzisha kampeni yake kwa jina “Simama Uhesabiwe; Uokoe Mukurwe-ini” kuhimiza watu wa eneo bunge hilo kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa.

Naye Gavana wa Pokot Magharibi, Profesa John Lonyangapuo ameitaka serikali kuhakikisha kuwa wakazi wa eneo hilo waliokwenda Uganda kutafuta lishe na maji kwa mifugo wao wanahesabiwa.

Wakati huo huo, kumeibuka malalamishi mengi kuhusu uajiri wa maafisa watakaoendesha zoezi hilo.

Wakazi wa maeneo mbalimbali nchini wamelalamika kuwa kulikuwa na upendeleo katika kuajiri maafisa 135,000 wa kuhesabu watu.