Habari za Kitaifa

Utakachokatwa kwenye mshahara kwa ajili ya bima mpya ya SHIF ya Kenya Kwanza

January 19th, 2024 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

RAIS William Ruto ameendelea kupata anachotaka, huku uamuzi wa jana wa Mahakama ya Juu kuhusu Bima ya Afya ya jamii (SHIF) ikiwa sehemu ya mteremko anaoendelea kupata mahakamani.

Jana, majaji wa mahakama hiyo walimruhusu Rais Ruto awabebeshe Wakenya mzigo zaidi, walipobatilisha agizo la mahakama kuu iliyokuwa imezuia ushuru huo wa asilimia 2.75.

Kabla ya uamuzi wa jana, Rais Ruto alikuwa ameapa kuendelea kuwatoza ushuru kugharamia miradi aliyoanzisha, hata ikiwa mahakama itatoa maagizo ya kupiga marufuku kodi zinazopitishwa na bunge na kuzitia sahihi ziwe sheria.

Rais Ruto amepata mteremko mahakamani baada ya malumbano ya hivi punde na idara ya mahakama akidai kuna majaji wafisadi wanaosimamisha miradi ya maendeleo kwa kutoa maagizo ya kupiga breki miradi ya maendeleo na kwamba atapambana nao.

Wachanganuzi wa masuala ya sheria na siasa wanaamini maamuzi mengi yajayo yataipendelea serikali, kutoka na Rais Ruto kuwatisha na kuwatia woga majaji.

Uamuzi wa jana si wa kwanza kwenda upande wa serikali. Licha ya Mahakama kuu kuharamisha utozwaji wa asili mia moja nukta tano (1.5 ya kodi ya nyumba, Mahakama ya Rufaa ilizima agizo hilo na kuruhusu kodi iendelee kutozwa wananchi.

Kodi nyingine ambayo ilizua tumbojoto na kusababisha Rais Ruto kuwakemea majaji hadharani baada ya kusitishwa na Jaji Enock Chacha Mwita, ni hii ya bima ya afya (SHIF). Majaji wa Mahakama ya Rufaa Patrick Kiage, Pauline Nyamweya na Grace Ngenye Macharia baadaye waliamuru iendelee kulipwa.

Kodi nyingine ambayo inayosababisha mtafaruku baina ya waajiri na wafanyakazi ni ile ya hazina ya malipo ya uzeeni (NSSF) iliyoongezwa kati ya Sh200 na Sh2000 kila mwezi.

Sio kodi pekee ambazo Rais Ruto amezichangamkia bali pia kesi za wandani wake kati ya kesi hizo ni ile ya ufisadi ya Sh7.3 bilioni iliyomkabili Naibu Rais Rigathi Gachagua na washtakiwa wengine.

Kesi hiyo ilitamatishwa, na Bw Gachagua akaachiliwa huru.

Wengine waliofaidi na utawala wa serikali ya Kenya Kwanza ni aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich. Aliondolewa mashtaka ya ufisadi wa Sh63 bilioni katika kashfa ya mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Mawaziri wa Kenya Kwanza walioshtakiwa na sasa wako huru ni; Mithika Linturi (kesi ya dhuluma za kimapenzi) na Aisha Jumwa (kesi ya mauaji na ufisadi).

Waliokuwa wakuu wa kampuni ya Kenya Power na Kenya Pipeline, Mabw Ben Chumo na Joe Sang mtawalia, waliachiliwa katika kesi za ufisadi.

Ingawa mahakama ilizima harakati zozote kuhusu Ushuru wa Nyumba za Bei Nafuu, serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wananchi.

Katika kesi malipo ya ada ya bima ya afya Majaji Kiage, Nyamweya na Macharia walisema sasa sheria tatu mpya zilizobuni SHIF zianze kutumika.

Sheria hizi ziliopitishwa Desemba 2023.