Habari MsetoSiasa

Utakuwa mlima kwa Ruto kupenyeza magharibi – Wandani wa Mudavadi

October 18th, 2018 2 min read

Na DERRICK LUVEGA

VIONGOZI wanaomuunga mkono kinara wa ANC Musalia Mudavadi, wameapa kumtoa kijasho Naibu Rais William Ruto katika harakati zake za kujipenyeza kisiasa katika eneo la magharibi kusaka kura kuelekea 2022.

Viongozi hao hususan kutoka kaunti za Vihiga na Kakamega pia walihimiza wafuasi wao kote nchini kujitayarisha kwa kivumbi kati ya Bw Mudavadi na Bw Ruto kwenye kinyang’anyiro cha urais 2022.

Bw Ruto amezuru eneo la magharibi mara kadha huku ziara ya hivi punde ikiwa Ijumaa iliyopita ambapo alifanya mikutano ya umma mjini Bungoma, Kakamega na Vihiga siku hiyo hiyo.

Mbunge wa Sabatia Alfred Agoi, ambaye ni mwandani wa Bw Mudavadi, alisisitiza kuwa hawatakubali ushawishi wowote kujiunga na Bw Ruto.

Alisema: “Kinyang’anyiro cha 2022 ni baina ya Mudavadi na Ruto. Ruto anazurura huku akimwaga pesa na kutoa ahadi za maendeleo ili kuwafumba macho wananchi.

“Utakapowadia wakati wa kupiga kura ndipo tutajua mbivu na mbichi. Ziara za Ruto hazitafua dafu kama ilivyokuwa kabla ya uchaguzi wa 2017. Alipiga kambi hapa mara kadha lakini hakupata kura zozote.”

Mwakilishi wa Wanawake Vihiga Beatrice Adagala alimsuta Naibu Rais kwa kuzindua taa za barabarani Vihiga, akisema ni hatua ya kuwafumba macho wenyeji kwamba analeta maendeleo katika kaunti hiyo. Aliwaomba wapiga kura wampuuze Bw Ruto na zawadi zake.

“Ni wazi kwamba lengo ni kuwapumbaza watu wetu ili wamuunge mkono. Hatutakubali kamwe hilo. Tunaomba watu wetu kumuunga mkono Bw Mudavadi,” akasema Bi Adagala.

Bw Mudavadi, ambaye alikuwa Makamu wa Rais zamani na kisha Naibu Waziri Mkuu, aliwania urais mara ya mwisho 2013 na kuzoa kura 450,000 pekee.

Mwaka 2017, alimuunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga chini ya muungano wa National Super Alliance (NASA).

Hata hivyo, tangu muafaka wa kisiasa kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, hajazungumzia suala la uchaguzi 2022 na badala yake amekuwa akihimiza umoja wa jamii ya Waluhya – jambo ambalo limekuwa gumu kutimia kwenye msururu wa chaguzi zilizopita.

Hivi majuzi, wabunge kadha wa magharibi walikutana na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi. Bi Adagala hakuhudhuria.

Jumatano, alidinda kutoa sababu za kukosa mkutano huo akisisitiza kuwa hataki kuwa sehemu ya mradi wa kumpigia debe Naibu Rais Bw Ruto.

Mkutano mwingine umepangiwa kufanyika Oktoba 19 katika Ikulu ya Kakamega, siku moja tu kabla ya sherehe za Mashujaa zitakazoandaliwa kwenye uwanja wa michezo wa Bukhungu.

Bw Mudavadi anatarajiwa kuhudhuria sherehe hizo zitakazoongozwa na Rais Kenyatta.

Viongozi kadha wa Ford Kenya wakiongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, naibu wake Boni Khalwale na mbunge wa Kimilili Chris Wamalwa, walijumuika na Bw Ruto katika ziara yake Ijumaa eneo la magharibi na kuelezea kumuunga mkono.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula ameeleza kuwa haungi mkono azma ya Naibu Rais kuwania uongozi wa taifa akisema yeye pia atawania urais.