Habari za Kitaifa

Utangazaji wa Matokeo ya KCSE wagatuliwa na kupelekwa jiji la Rais Ruto, Eldoret

January 8th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

Ni mara ya kwanza matokeo ya Mitihani ya Kitaifa ya Shule ya Sekondari nchini (KCSE) kutangazwa kutoka nje ya jiji la Nairobi.

Maafisa wa Wizara ya Elimu walitangaza matokeo haya katika Shule ya Upili ya Moi Girls jijini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Asanteni kwa sababu tuliwapa notisi fupi muandae jumba hili bila kujua ilikuwa kwa sababu gani na mkafanya kazi nzuri,” alieleza Katibu wa Wizara ya Elimu Prof Belio Kipsang akipongeza uongozi wa shule hiyo.

Ilivyo desturi ya muda mrefu, matokeo ya mitihani ya kitaifa hutolewa kwa umma kutoka Taasisi ya Ustawishaji Mtaala nchini (KICD) na makao makuu ya Baraza la Mitihani ya Kitaifa nchini (KNEC).

“Ninashukuru sababu umegatua matangazo ya KCSE hadi hapa Eldoret na si kwa vile nilisomea hapa,” alisifu Seneta Maalum Prof Margaret Kamar.

Kabla ya kutangaza matokeo ya KCSE, Waziri Ezekiel Machogu alimjulisha Rais William Ruto katika Ikulu ndogo ya Eldoret.

Yamkini matangazo haya yametolewa kutoka Eldoret sababu Rais yuko Kaunti ya Uasin Gishu kwa ziara ya kikazi.