Makala

AKILIMALI: Utaratibu mwafaka wa kukuza nyasi kwa ajili ya mauzo

March 21st, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KWA mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Ubora wa Mimea KEPHIS pamoja na KARI, nyasi za Nappier ni miongoni mwa mimea inayotegemewa sana kama lishe kwa mifugo katika maeneo yanayopokea kiasi kikubwa cha mvua.

Aina hii ikiwa aina mojawapo ya nyasi zinazokua kwa haraka sana bila ya gharama kubwa za upanzi, Nappier hupandwa kwa kutumia magugu yanayoweza kuchimbiwa mchangani na (au) kufukiwa katika mashimo yenye urefu wa hadi kufikia inchi sita kama mimea mingine.

Ili mimea iweze kuchomoka kwa kimo cha kutoshana, kuna haja kubwa ya mkulima husika kutumia mbinu za kisasa zilizo rahisi na nyepesi zaidi kumudu.

Mara mashina (shoots) yanapochomoka kutoka ardhini, mkulima anafaa kuyakata inchi sita kutoka kwenye udongo kwa mashine maalumu iitwayo Nappier Cutter.

Mtambo huu una uwezo wa kulainisha mimea hii katika shamba zima bila ya kuathiri ukuaji wala mfumo wa uzalishaji bora wa kila mmea.

Pili, mkulima anastahili ahakikishe kwamba kuna usawazishaji wa mbolea mwafaka hasa zile zitokanazo na majani yaliyooza au samadi katika shamba zima kwa kunyunyizia dawa ya kuangamiza magugu ya kwekwe yaani ‘Kikuyu Grass’ yanayoweza kushambulia mimea na hivyo kuathiri mazao.

Hatimaye, ni sharti mkulima kuchanganya mbolea za kisasa na zile zinazotokana na mazao ya shambani ili kupunguza kiwango cha asidi katika mchanga na tindikali inayoweza kukolea katika mimea hii.

Uangalizi wa mara kwa mara ni muhimu sana. Bw Zack Gichohi amekuwa mzalishaji wa miche yake pamoja na upanzi katika shamba la ekari nne tangu miaka ya themanini.

Anasema kilimo chake kina faida nyingi kwa upande wa biashara na hata kwa mifugo alionao pembeni mwa shamba lake.

Maji

Anasimulia kuwa mimea yake haihitaji kiwango kikubwa cha maji au mvua kwani miche yake imefanyiwa uchanganyaji wa mimea ‘Cross Breeding’ na ile inayokua katika maeneo yenye ukavu haiathiriwi na jua kali.

Mfumo wa ukataji pia unategemea maeneo.

Kila sehemu hukatwa katika siku maalumu ili kutoa nafasi kwa nyasi hizi kukua kwa haraka bila ya usumbufu.

Matawi yake lazima yanyooke kuelekea juu ila tu yanapokumbwa na maradhi ndipo yanaweza kupinda au kunyauka. Ukuaji wake unahitaji mchanga wenye kiwango cha PH 2-4.5.

Inaelezwa kuwa, kiwango hiki cha asidi ndicho huipa mimea hii ugumu unaoweza kucheuliwa vizuri na wanyama tumboni.

Hii humpa mnyama lishe bora inayochangia upatikanaji wa madini muhimu ya Potassium katika maziwa.

Kila baada ya wiki moja, kimo cha nyasi ya nappier huongezeka kwa inchi mbili hivyo basi mavuno maridhawa ni kila baada ya wiki tatu kwa wale wanaojihusisha na uuzaji wa mimea hii.

“Kila baada ya wiki tatu, ninapata mavuno mengi kabla ya kukata upya mashina hadi kimo nilichoshauriwa,” anasema Gichochi.