Habari

Utaratibu wa uteuzi wa Mkaguzi Mkuu mpya kuanzia Septemba 23

August 28th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

JOPO la kuwapiga msasa watakaotuma maombi ya kujaza nafasi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali litateuliwa mnamo Septemba 23, 2019.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye alianzisha mchakato wa uteuzi wa atakayechukua wadhifa huo kwa kutangaza wazi nafasi hiyo kupitia notisi kwenye gazeti rasmi la serikali Jumanne siku moja baada ya Edward Ouko kukamilisha muhula wake wa kuhudumu Jumatatu.

Rais atateua mwenyekiti wa jopo hilo la uteuzi pamoja na wanachama ambao watatoka Hazina ya Kitaifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Utumishi wa Umma, Taasisi ya Wahasibu Nchini (ICPA), Muungano wa Mashirika ya Kitaalamu Afrika Mashariki na Chama cha Wanasheria Nchini (LSK).

Hii ni kulingana na Sehemu ya 11 (5) ya Sheria kuhusu Ukaguzi wa Asasi za Umma ya 2015 (Public Audit Act 2015).

Kwa mujibu wa notisi hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali, wale ambao wanataka kushikilia wadhifa huo wamepewa muda wa hadi Septemba 9, 2019, kuwasilisha maombi yao.

Bw Ouko aliteuliwa kuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa kwanza chini ya Katiba ya sasa, mnamo Agosti 27, 2011, na Rais mstaafu Mwai Kibaki.

Kulingana na sehemu ya 11 (3) ya Sheria kuhusu Ukaguzi wa Asasi za Umma, wanaotuma maombi kwa uteuzi kuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wanahitajika kuyawasilisha kwa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) au kupitia mashirika au makundi yanayounga mkono azma zao.

“Barua za maombi chini ya ibara ya (2) zitawasilishwa kwa Tume ya Kuwaajiri Watumishi wa Umma (PSC) siku 14 baada ya notisi kutolewa kuhusu uwepo wa nafasi katika Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Na maombi hayo yawasilishwe na; (a) mtu aliyehitimu; (b) mashirika au makundi yanayounga mkono uteuzi wa yeyote aliyehitimu,” sheria hiyo inasema.

Wanaotuma maombi kwa wadhifa huo wanapaswa kuwa na sifa kadhaa muhimu zikiwemo; “ujuzi na uelewa mpana katika masuala kuhusu Fedha za Umma au angalau tajriba ya miaka 10 na zaidi katika taaluma ya ukaguzi wa matumizi ya fedha katika asasi za umma au usimamizi wa fedha za umma”.

Kuhoji

Jopo la uteuzi linahitajika kuendesha vikao vya kuwahoji waliowasilisha maombi hadharani. Baadaye litateua majina ya watu watatu na kuwayawasilisha kwa Bunge pamoja na alama walizopata wote waliohojiwa.

Orodha hiyo ya watu watatu pia itawasilishwa kwa Rais ambaye atateua mmoja ndani ya muda wa siku saba baada ya ofisi yake kupokea majina hayo.

Mtu atakayeteuliwa na Rais kuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali sharti aidhinishwe na Bunge la Kitaifa baada ya kupigwa msasa na wabunge kwa kipindi cha siku saba.

Kipengee cha 229 (4) cha Katiba ya sasa kinampa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mamlaka ya kukagua matumzi ya fedha katika asasi za umma na kuwasilisha ripoti zake ndani ya muda wa miezi sita baada ya kila mwaka wa kifedha.

Hukagua stakabadhi za matumizi ya fedha katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

Mkaguzi wa Hesabu za Serikali pia hutoa ripoti za ukaguzi wa matumizi ya fedha katika mashirika ya serikali na idara za serikali katika serikali kuu na zile za kaunti, akaunti za mahakama zote za Kenya, tume na ofisi huru, akaunti za Bunge la Kitaifa na Seneti pamoja na vyama vya kisiasa ambavyo hufadhiliwa kwa pesa za umma.

Vilevile, ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hukusanya maelezo na kuandaa ripoti kuhusu deni la kitaifa.