Habari

Utata kando, mipango ya mazishi ya Ken Okoth kuendelea

August 2nd, 2019 3 min read

Na MAUREEN KAKAH na MARY WANGARI

MIPANGO ya mazishi ya mbunge Ken Okoth kuendelea baada ya mahakama kukubali hati ya makubaliano iliyotiwa saini baina ya mjane Monica Okoth na diwani Anne Thumbi hivyo kutanzua mkwamo uliotishia kuvuruga mambo.

Kwenye hati hiyo ya makubaliano iliyowasilishwa katika Mahakama ya Masuala ya Ajira na Leba, Bi Okoth na Bi Thumbi wamekubaliana chembechembe zichukuliwe kupima vinasaba (DNA) kubainisha ikiwa marehemu ni baba mzazi wa kijana ambaye ni mtoto wa diwani huyo.

Wawili hao wamekubaliana mtoto aliyetajwa ashiriki kikamilifu katika mipango ya mazishi.

Bi Thumbi alikuwa amewasilisha kesi mahakamani Alhamisi wakati wa ibada ya Okoth ikiendelea Kibra. Alitaka suala la kuondoa utata kuhusu baba mzazi wa mwanawe litatuliwe.

Kulingana na Dunstan Omari, wakili anayemwakilisha Thumbi, uamuzi huo uliafikiwa kufuatia mazungumzo yaliyoendelea hadi usiku wa manane yaliyoongozwa na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga.

Omari pia alidokeza kwamba chembechembe za kufanyia uchunguzi wa DNA zilitarajiwa kutolewa kutoka kwa mwili wa mbunge wa Kibra kufikia saa kumi jioni, mnamo Ijumaa, Agosti 2, 2019, ambapo pande zinazozozana zitahitajika kutoa mpasuaji wao binafsi wao kila mmoja.

“Shughuli ya kuuteketeza mwili itaendelea jinsi ilivyopangwa lakini baada ya kutoa chembechembe za kufanyia uchunguzi wa DNA kutoka kwenye mwili wa Mbunge Ken Okoth katika mochari ya Lee Funeral Home. Hatujalala. Leo tumeafikiana,” alisema wakili huyo.

Isitoshe, alisema lilikuwa suala la kifamilia akifichua kwamba hakukuwa na mgogoro kuhusu namna ya kuuzika mwili wa Okoth wala kuhusu ugavi wa mali yake.

Wakili Ediwn Sifuna anayemwakilisha mamake Okoth, Angelina Okoth na mkewe Monica Okoth alisema hawakuwa na pingamizi yoyote dhidi ya kufanya uchunguzi wa DNA.

“Nina furaha kwamba kunaonekana mwanga hatimaye, tunaelekea Lee Funeral Home kusuluhisha masuala yote yaliyosalia,” alisema akiongeza kwamba Jayden Baraka Okoth, anayedaiwa kuwa mwanawe Okoth, ataruhusiwa kushiriki mipango ya mazishi hayo.

Alikuwa amemshtaki mama mzazi wa Okoth ambaye ni Bi Angeline, mjane Monica, na mochwari ya Lee Funeral Home mtawalia.

Kichekesho cha Millie Odhiambo

Huenda wanaume wakashurutishwa kuweka wazi idadi ya watoto waliozaa ndani na nje ya ndoa wakiwa wangali hai iwapo Mbunge wa Suba Kaskazini, Bi Millie Odhiambo atatimiza ahadi yake ya kuwasilisha mswada kuhusu suala hili.

Mnamo Alhamisi, Agosti 1, mwanasiasa huyo anayefahamika kwa ujasiri wa kuelezea hisia zake, alijitosa mtandaoni na kutangaza kwamba atawasilisha mswada utakaowalazimu wanaume kufichua hadharani wakiwa bado hai kuhusu watoto wao katika ndoa na nje ya ndoa, ili kuzuia visanga vinavyozuka wakati wa maombolezi na mazishi.

“Ninawasilisha mswada wa kufanyia marekebisho Sheria kuhusu Ndoa kuwashurutisha wanaume wote kuwatangaza hadharani watoto wao waliozaa ndani na nje ya ndoa wakiwa wangali hai, na wakikosa kina mama zao watangaze. Kuomboleza huku ukikumbwa na matukio ya ghafla ya kushtusha kunaweza kusababisha matanga mengine,” alisema mwanasiasa huyo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.

Ni kauli iliyoibua hisia mbalimbali mitandaoni huku baadhi ya watumiaji mitandao hiyo wakimuunga mkono na wengine wakitofautiana naye wakiandika kwamba hatua hiyo huenda ikavunja ndoa nyingi.

Hisia zake zilijiri baada ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuacha waombolezaji waliokusanyika katika ibada ya kumuaga buriani marehemu Ken Okoth vinywa wazi baada ya kupasua mbarika kuhusu mpenzi wake wa siri, Anne Muthoni Thumbi ambaye inadaiwa walizaa naye mtoto mmoja.

“Mimi ni shahidi kuhusu haya. Nitakuwa nimemhini Ken kwa kukaa kimya kuhusu haya kwa sababu ninajua ukweli. Walikuwa na uhusiano na hata mara ya mwisho walikuwa Ufaransa pamoja. Ninamhurumia Monica, ninajua ni mjane wakati huu mgumu lakini acheni niseme ukweli,” Sonko alitoboa siri huku baadhi ya waombolezaji wakimshangilia.

Mahakama mnamo Alhamisi, Agosti 1, ilimpa Thumbi, ambaye pia ni diwani katika Baraza la Kaunti ya Nairobi, idhini ya kusimamisha shughuli za mazishi ya Mbunge huyo wa Kibra, baada ya kuwasilisha kesi akilalamikia dhidi ya kutengwa pamoja na mwanawe katika shughuli za mazishi, na familia ya Okoth.

Aidha, katika kesi hiyo ambayo ilitengewa tarehe ya kusikizwa mnamo Agosti 9, Thumbi aliwasilisha masharti matatu ambayo alitaka mamake Okoth, Bi Angelina Okoth na mjane Bi Monica Okoth, kutimiza kabla ya kuendelea na shughuli ya mazishi.

Pia alikuwa ameishtaki mochwari ya Lee Funeral Home.