Habari Mseto

Utata kuhusu safari za Mecca Waislamu wakikosa paspoti

July 18th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

ZAIDI YA Wakenya 2,000 waumini wa dini ya Kiislamu  huenda wakakosa kwenda Hijjah mjini Mecca  hata baada ya serikali ya Saudia Arabia kuwaruhusu kutokana na kukosa kupokea paspoti na kupitishwa kwenye ukaguzi mgumu na maafisa wa idara ya uhamiaji.

Hii ni baada ya wengi wa waumini hao kulalamika kwamba wamepigwa kumbo na uongozi wa Baraza la dini ya Kiislamu nchini SUPKEM ambao wamedai wanasaidia tu wale wanaogharamia safari zao kupitia maajenti wao.

“Mimi nilituma ombi la kupewa pasipoti miezi mitano iliyopita na nimezungushwa ya kutosha mpaka nikachoka. Nimeenda SUPKEM lakini waliniandikia barua tu na kunituma kwa ofisi za idara ya uhamiaji wanasaidia tu watu waliotumia maajenti wao. Mimi sina pesa za kulipa ajenti.,” akaeleza Bi Aisha Salim ambaye alisema kwamba alipofika katika ofisi za idara ya uhamiaji aliambiwa faili yake haionekani wala maelezo yake hayako mtandaoni.

Kando na Bi Aisha, visa vya malamishi kuhusu kutopata cheti cha pasipoti vimekuwa vingi na sasa wanamwomba Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati ili waweze kupata vyeti hivyo  ndipo wasafiri na kutimiza nguzo hiyo ya tano katika dini ya kiislamu.

Huku hayo yakiendelea,  uongozi wa SUPKEM  na Muungano wa Hajj na Umra Kenya wametofautiana vikali kuhusu matayarisho ya hijjah

Katibu mpanga ratiba  wa SUPKEM Abdullahi Salat amepuuzilia mbali taarifa za awali kutoka kwa muungano wa Hajj na Umra Kenya kwamba makataa ya kulipa ada ya tiketi ya ndege, malazi, vyakula na mambo mengine muhimu yamesongeshwa mbele hadi tarehe 31 mwezi huu.

Bw Salat badala yake amemshtumu vikali Mwenyekiti wa Muungano wa Hajj na Umra Kenya Sharrif Husein ambaye alikuwa katika uongozi wa SUPKEM mwaka uliopita kwa kuwapotosha Waislamu ilhali hana mamlaka ya kuzungumza kwa niaba yao.

“Sisi hatujabadilisha safari wala makataa ya malipo. Tayari watu 4361 wamekamilisha mchakoto mzima wa malipo ila swala la pasipoti kwa baadhi yao bado linashughulikiwa na idara ya uhamiaji nchini,” akasema Bw Salat.

Aidha alidai kwamba tayari watu 4361 wamelipa pesa zinazohitajika lakini kizingiti kilichosalia kwa baadhi yao ni kupokezwa pasipoti.

Hata hivyo Bw Hussein ambaye alionyesha nyaraka na idhini kutoka kwa Waziri wa Hajj nchini Saudi Arabia Mohamed Swaleh zilizoruhusu kusongeshwa kwa makataa hayo aliwalaumu viongozi wa SUPKEM kwa kutomakinikia safari za hijjah na kuwaomba Waislamu kutokumbwa na taharuki kuhusu safari hizo.

“Sisi kama muungano tulimwandikie waziri wa Hajj nchini Saudia barua na akaitikia kwamba makataa hayo yasongeshwe ili waumini wengi wasifungiwe nje. Tunawomba mahujaji wote wajitayarishe  ili kufikia mwisho wa mwezi huu wawe wametimiza mahitaji yote,” akasema Bw Hussein.

Kwa upande wake Msemaji wa wizara ya usalama wa ndani Mwenda Njoka alikanusha kupokea habari zozote kutoka kwa uongozi wa SUPKEM kuhusu malalamishi ya kujikokota katika mchakato wa kupeana pasipoti au ubaguzi.

“Ni mara ya kwanza nasikia kuhusu malalamishi hayo. Kuna utaratibu wa kufuata na ukaguzi ndipo pasipoti zitolewe. Ikiwa hayo yamefuatwa basi sijui kwa nini lalama hizo ambazo zijasikia awali sasa zinaibuka,” akaeleza Bw Njoka.

Majuma matatu yaliyopita viongozi wa SUPKEM waliwaeleza wanahabari kuhusu changomoto za mahujaji kucheleweshewa pasipoti zao na hata kutoa wito kwa idara ya uhamiaji kuharakisha shughuli hiyo.