Habari

Utata shuleni muhula ukianza

December 31st, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SHULE zinatarajiwa kufunguliwa kuanzia Alhamisi wiki hii huku kukiwa na utata kuhusu masuala kadhaa ambayo huenda yakaathiri masomo.

Walimu wametishIa kugoma na kususia utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ambao serikali inasema ni lazima uanze kutumika mwaka huu. Walimu wanasema mtaala wa 2-6-6-3 unahitaji kupigwa msasa kwanza kabla ya kuanza kutekelezwa.

Masomo yanaweza kuathiriwa iwapo walimu watagoma serikali isipobatilisha uhamisho wa walimu, kuwapandisha vyeo na kukubali matakwa yao ya kuendelea kujiimarisha kikazi. Kwenye ilani kwa walimu jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Bw Wilson Sossion alisema:

“Mnafahamishwa kwamba mgomo utaanza tarehe ya kufunguliwa kwa shule na hakuna mwalimu anayepaswa kuripoti kazini hadi mgomo utakapofutiliwa mbali na katibu mkuu kufuatia azimio na Baraza Kuu la chama.”

Kulingana na walimu, itakuwa vigumu kutekeleza mtaala huo kukiwa na mapengo yaliyotajwa na wataalamu walioutathmini. Waziri wa Elimu, Amina Mohammed, anasisitiza kuwa mtaala huo utaanzwa kutekelezwa kwa awamu shule zikifunguliwa Alhamisi ilivyokuwa imepanga serikali.

Bi Mohammed alikuwa ametilia shaka utekelezaji wa mtaala huo kuanzia mwaka ujao hadi utakapopigwa msasa kabla ya kubadilisha msimamo na kutangaza kwamba lazima utatekelezwa.

Kulingana na waziri, alishauriana na wadau katika sekta ya elimu yakiwemo mashirika ya kidini, Taasisi ya ukuzaji wa mitaala (KICD), Tume ya Walimu (TSC), Baraza la Kitaifa ya Mitihani (KNEC) na Wachapishaji wa vitabu nchini (KPA).

Hata hivyo, kulingana na Bw Sossion, walimu ambao wanapaswa kufanikisha utekelezaji wa mtaala huo hawakushauriwa. “Ni makosa kulazimisha mtaala huu wakati ambao tumefahamishwa udhaifu wake. Tunahitaji kuupiga msasa kwanza, pengine mwaka ujao, kabla ya kuanza kuutekekeza kitaifa,” alisema Bw Sossion.

Mnamo Oktoba, KICD ilitoa ripoti kuonyesha kuwa walimu hawajaandaliwa vyema kufanikisha mtaala huo.

Ripoti hiyo ilisema kwamba baadhi ya walimu hawana uwezo unaohitajika kufanikisha mtaala huo mpya na shule nyingi hazina vifaa vinavyohitajika kuutekeleza. Wazazi wengi wanasema siku tatu kabla ya shule kufunguliwa kwa muhula wa kwanza wa mwaka, hawajui vitabu ambavyo watanunua.

Aidha, wanalalamikia tarehe ya kufungua shule za msingi wakisema inakaribiana na ya kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza ambayo ni wiki ijayo.

Kulingana na wazazi, muhula unaanza punde tu baada ya msimu wa sherehe ambapo kuna matatizo ya usafiri. Baadhi ya walimu wanasema hawakuweza kuwapa wazazi orodha ya vitabu vya kununua kufuatia utata uliogubika utekelezaji wa mtaala huo.

Akihojiwa na wanahabari mjini Mombasa Alhamisi wiki jana, Rais Uhuru Kenyatta alikiri kwamba serikali imekuwa ikikanganya Wakenya kuhusu utekelezaji wa mtaala huo na akaomba msamaha.