Habari Mseto

Utata wagubika kiini cha kifo cha mwalimu mkuu

November 19th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

USIMAMIZI wa Shule ya Upili ya Oyugi Ogango iliyoko eneobunge la Rongo, kaunti ya Migori umekana madai kuwa Mwalimu Mkuu Bi Martha Ouma alifariki kutokana na ugonjwa hatari wa Covid-19.

Hata hivyo, utawala wa eneo hilo umesema haijapata ripoti kuhusu kiini cha kifo hicho.

Lakini kwa mujibu wa naibu wa mwalimu mkuu Roseline Abama bosi wake alikuwa akipokea matibabu katika hospitali moja mjini Kisumu kwa muda wa wiki moja akiwa na matatizo ya kifua.

“Tumetamaushwa na kifo cha mwalimu wetu kwa kuwa amekuwa na afya nzuri hadi wiki jana ambapo alipelekwa hospitalini Kisumu akiwa na tatizo la kifua”,akasema Bi Abama.

“Aidha tungetaka kukana vikali uvumi ambao umekuwa ukinea kwamba mwalimu mkuu wetu alifariki kutokana na maradhi ya Covid-19. Rekodi za daktari ambazo tuko nazo zinasema kuwa alifariki kutokana na matatizo ya kifuo” akaongeza.

Bi Abama alihimiza wazazi, walimu na wanakiji wa eneo hilo kuwa na utulivu kwa kuwa hakuna kitu cha kuogofya.

Kwa upande wake naibu wa kamishna wa kaunti ndogo ya Rongo Andrew Mwiti ambaye pia alizuru shuleni humo baada ya tukio hilo alidokeza kuwa masharti yote ya kupambana na usambazaji wa maradhi ya corona yalifuatwa akitofautiana na uvumi huo wa kifo cha mwalimu huyo aliugua Covid-19.

“Hatuwezi kusema kuwa mwalimu huyu amekuwa akiugua corona kwa kuwa hatujaona ripoti kutoka kwa daktari na hospitali ambako amekuwa akitubiwa kule Kisumu. Pindi tutakapopata ripoti hiyo ndipo tunaweza kutangaza kiini cha kifo chake akasema Bw Mwiti.

Aidha aliongeza kuwa bado wanashirikiana na Wizara ya Afya kuimarisha shughuli ya upimaji virusi vya corona katika idara mbalimbali za serikali katika eneo hilo pamoja na shule kadha njia mojawapo ya kudhibiti msambao wa virusi vya corona.

Kaunti ndogo ya Rongo sasa ndio inaongoza kwa visa vya maambukizi ya Covid-19 katika kaunti ya Migori.

Wakati huo huo, risala za rambi rambi bado zinazidi kufuatia kifo cha Bi Ouma ambaye amehudumu kama mwalimu mkuu katika shule hiyo kwa zaiid ya miaka minane.

Miongoni mwa walituma risala zao ni Mbunge wa Rongo Bw Paul Abuor alimtaja marehemu kama mwalimu ambaye mchapa kazi na ambaye alishirikiana na viongozi na wadau wa elimu katika eneo kuinua viwango vya masomo katika Shule ya Upili ya Oyugi Ogango.