Habari

Utata wakumba mpango wa Rais kuhusu hatimiliki

November 23rd, 2020 1 min read

PETER MBURU na BRIAN WASUNA

MATUMAINI ya watu zaidi ya 25,000 ambao walitarajia kunufaika na agizo la Rais Uhuru Kenyatta kuhusu ukabidhi wa hati za kumiliki ardhi, yamefifia baada ya kubainika kuwa, baadhi ya ardhi zilizolengwa zina hati zaidi ya moja.

Ardhi hizo ziko katika eneo la Ruai chini ya kampuni ya Embakasi Ranching.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibainisha kuwa, katika baadhi ya vipande vya ardhi, Wizara ya Ardhi iliharakisha kutoa hati za umiliki bila kukamilisha uchunguzi jinsi inavyohitajika kisheria.

Matokeo yake ni kwamba, baadhi ya hati miliki zinazokabidhiwa kufuatia amri ya Rais huenda zikawa karatasi tupu bila umuhimu wowote kwani tayari kuna wamiliki waliokuwa wamepewa hati awali.

Masoroveya wanaohusika katika mpango huo ambao tuliwahoji, walikadiria kwamba kuna takriban vipande 12,000 vya ardhi ambavyo vimeibua wasiwasi kuhusu uwezekano kwamba vilikuwa tayari vinamilikiwa na watu zaidi ya mmoja.

Kinachoibua hofu zaidi ni kuwa, majina ya watu yaliyotumwa ambao wanatakikana kupewa hati za umiliki ni mengi kuliko vipande vya ardhi vilivyopo.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi, Bi Farida Karoney alipuuzilia maswala hayo kama “uvumi” na kutaka aonyeshwe angalau hati kumi za umiliki ardhi ambazo zilitolewa bila ardhi hizo kuchunguzwa kwanza.

Alisisitiza uchunguzi ulifanywa kikamilifu kwa mujibu wa sheria kubainisha umiliki wa ardhi kabla hati kutolewa.