Utata zaidi kuhusu mustakabali wa Messi kitaaluma Barcelona ikienda kortini kuzuia uhamisho wake hadi PSG

Utata zaidi kuhusu mustakabali wa Messi kitaaluma Barcelona ikienda kortini kuzuia uhamisho wake hadi PSG

Na MASHIRIKA

MPANGO wa Lionel Messi kuingia katika sajili rasmi ya Paris Saint-Germain (PSG) umekumbwa na utata zaidi baada ya mawakili wa Barcelona kuenda mahakamani kuzuia uhamisho wa fowadi huyo raia wa Argentina.

Tukio hilo linajiri siku chache baada ya Messi kuagana rasmi na Barcelona na kudokeza kwamba ameafikiana na PSG wamsajili kwa mkataba wa miaka miwili.

Kwa mujibu wa Barcelona, uhamisho wa Messi hadi PSG utakiuka kanuni za matumizi ya fedha miongoni mwa klabu (Financial Fair Play) na kushusha viwango vya ushindani na kuyeyusha ladha ya soka ya bara Ulaya.

“PSG hawastahili kabisa kumsajili Messi. Mnamo 2019-20, asilimia 99 ya mapato yote ya PSG ilitumiwa kugharimia mishahara huku Barcelona ikitumia asilimia 54 pekee,” ikasema sehemu ya barua ya malalamishi iliyowasilishwa na Dkt Juan Branco katika Mahakama ya Rufaa ya bara Ulaya kwa niaba ya Barcelona.

Jaribio hilo la Barcelona huenda sasa likavuruga au kuchelewesha zaidi mchakato wa Messi kutua PSG – kikosi kinachojivunia maarifa ya baadhi ya wanasoka ghali zaidi duniani.

Kwa upande wao, PSG wanashikilia kwamba uhamisho wa Messi hadi kambini mwao hautakiuka kanuni za matumizi ya fedha kwa mujibu wa sheria za Uefa kwa sababu wengi wa masogora waliojiunga na klabu hiyo muhula huu walifanya hivyo bila ada yoyote.

Mmoja wao ni aliyekuwa kipa chaguo la kwanza kambini mwa AC Milan, Gianluigi Donnarumma aliyesaidia Italia kunyanyua ubingwa wa Euro 2020. Wengine ni mabeki Achraf Hakimi na Sergio Ramos wanaotarajiwa kupangwa mara kwa mara na Presnel Kimpembe, Marquinhos Correa, Juan Bernat na Leandro Paredes kwenye kikosi cha kwanza.

Gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa, limesema PSG wako radhi kumpokeza Messi mshahara wa Sh312 milioni kwa mwezi. Huo ndio ujira ambao kikosi hicho kwa sasa kinamlipa Neymar Jr kila baada ya wiki nne.

Tangu atwae uenyekiti wa PSG mnamo 2011, Nasser Al-Khelaifi amefanikisha usajili wa wanasoka wa haiba kubwa wakiwemo Kylian Mbappe na Neymar aliyeagana na Barcelona kwa kima cha Sh26 bilioni mnamo 2017.

Kuingia kwa Messi kambini mwa PSG kutafanya mabingwa hao mara tisa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kuwa kikosi kinachojivunia wavamizi bora zaidi duniani.

Mbali na Mbappe, wafumaji wengine matata kambini mwa PSG kwa sasa ni Angel Di Maria na Neymar aliyewahi kucheza pamoja na Messi katika kikosi cha Barcelona kati ya 2013 na 2017.

Ingawa azma ya kutawala soka ya UEFA ndiyo ilikuwa sababu kuu ya kusajiliwa kwa Neymar, PSG wamekuwa wakibanduliwa mapema kwenye kampeni za kipute hicho.

Baada ya kulemewa na Bayern Munich kwa kichapo cha 1-0 kwenye fainali ya UEFA mnamo 2019-20, PSG ilidenguliwa na Manchester City msimu uliopita kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye nusu-fainali ya kipute hicho ambacho hawajawahi kukishinda.

Kwa mujibu wa wachanganuzi wengi wa soka ya bara Ulaya, maamuzi ya Messi kutua PSG kutachochea Mbappe anayewaniwa na Real Madrid ya Uhispania, kurefusha kandarasi yake ya sasa na kikosi hicho. Hata hivyo, hatua hiyo itazima ndoto ya kiungo Paul Pogba wa Manchester United kuingia katika sajili rasmi ya PSG.

“Kwa msingi wa kiuchumi, haiwezekani kwa PSG kuwadumisha Di Maria, Messi, Neymar, Mbappe na Pogba katika kikosi kimoja,” likasema gazeti la Mundo Deportivo.

Kati ya viungo mahiri watakaotegemewa na PSG kupiga jeki mashambulizi yao ni Marco Verrati na sajili mpya Giorginio Wijnaldum aliyeagana na Liverpool mwishoni mwa msimu jana.

Messi ambaye ni nahodha wa Argentina, aliagana rasmi na Barcelona mnamo Jumapili baada ya kuwajibikia miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa miaka 21.

Ingawa yalikuwa matamanio yake kusalia ugani Camp Nou kwa miaka mingine mitano, kigezo cha jinsi ambavyo Barcelona wangemudu mshahara kilizima maazimio yake.

Isitoshe, rais Joan Laporta alishikilia kuwa kumsaza Messi ugani Camp Nou kungeweka Barcelona katika hatari ya kuyumba kifedha kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50 ijayo.

Messi amekuwa mchezaji huru tangu Julai 1, 2021 baada ya mkataba wake kutamatika rasmi kambini mwa Barcelona. Sogora huyo ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Barcelona baada ya kufunga mabao 672 na kutwaa mataji 10 ya La Liga, manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na saba ya Copa del Rey. Anajivunia pia rekodi ya kunyanyua tuzo ya Ballon d’Or mara sita.

“Yasikitisha na bado sijaamini kwamba hutaweza tena kuchezea Barcelona,” akasema kocha wa Barcelona, Ronald Koeman.

“Najua matarajio ya kila mtu ni makubwa. Naamini tutafaulu pamoja kupeleka kikosi mahali ambapo kinastahili kuwa katika soka ya UEFA,” akasema kocha Mauricio Pochettino wa PSG.

Akisaidiwa na wakufunzi Jesus Perez na Miguel D’Agostino waliowahi kuhudumu naye kambini mwa Tottenham Hotspur, mwanasoka mwingine anayewaniwa na PSG kwa sasa ni kiungo raia wa Uingereza, Dele Alli wa Spurs.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wakulima Kiambu wapokea hundi ya Sh39 milioni kupiga jeki...

Polisi wapigana mmoja akimlaumu mwingine kwa kujisaidia...