Utawala wa Sossion katika KNUT hatarini

Utawala wa Sossion katika KNUT hatarini

Na SHABAN MAKOKHA

UTAWALA wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Walimu Kenya (KNUT) Wilson Sossion, sasa unaning’inia kwenye jabali baada ya kundi lililowahi kufanya kazi chini yake kuungana kwa lengo la kumtimua.

Mwenyekiti wa KNUT Collins Oyuu, ambaye anamezea mate wadhifa huo wa Katibu Mkuu, mnamo Jumamosi, aliwaongoza maafisa wengine wa muungano huo kufuatilia chaguzi za tawi la Mumias.

Waliwashawishi walimu kumkataa Bw Sossion debeni katika chaguzi zijazo za Kongamano la Wajumbe Maalum, ambapo maafisa wapya watachaguliwa.

Naibu wake Bw Sossion, Hesbon Otieno, alitangaza orodha mpya kwa jina “Team Change” (Timu ya Mabadiliko) ambayo inatarajiwa “kukomboa muungano huo ambao umevurugwa na utawala wa Bw Sossion.”

Kupitia ‘Team change,’ Bw Otieno alitangaza kuwa Bw Patrick Karinga kutoka Kisii Central atagombea wadhifa wa mwenyekiti ambapo nafasi ya makamu itawaniwa na Stanley Mutai kutoka Kericho kama naibu mwenyekiti wa kwanza na John Wesonga kutoka Mumias kama naibu mwenyekiti wa pili.

Bw Oyuu atawania cheo cha Katibu Mkuu huku Bw Otieno akiwania kiti cha naibu katibu wa kwanza na Bi Rosalia Mkwanjala kama naibu katibu wa pili.

Bw James Ndiku kutoka Makueni atagombea wadhifa wa mweka hazina, huku nafasi ya naibu ikigombewa na Ali Abdi kutoka Kaskazini Mashariki.

Bi Mercy Kiambati kutoka Mlima Kenya na Bi Mercy Ndungu kutoka Bonde la Ufa watakuwa wawakilishi wawili pekee wanawake huku Bw Edward Olando akiwakilisha walemavu.

Katibu Mkuu wa KNUT eneo la Magharibi Maurice Chalenga alisema eneo hilo limeafikiana kumuunga mkono Bw Oyuu kuchukua nafasi ya Bw Sossion, ambaye amekuwa akiongoza muungano wa walimu tangu 2013.

You can share this post!

Fumbo kuhusu mauaji ya mfanyabiashara Bashir

Wavuvi kuishtaki serikali upya kuhusu fidia