Habari Mseto

Utazimiwa simu ukikaidi kujisajili kwa Huduma Namba

April 18th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

SERIKALI imetishia kuwazimia wananchi simu zao ikiwa hawatakuwa wamesajili Huduma Namba kufikia siku ya mwisho ya kujiandikisha.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (CA) Francis Wangusi aliwaonya wananchi kuwa serikali haitakuwa budi kuzima njia zao za mawasiliano ikiwa hawatajiandikisha NIIMS.

Alisema watakaokataa kujiandikisha hawatakuwa na uwezo wa kutumia MPesa, Airtel Money na kutoa pesa kupitia kwa mashine au kupiga simu na kutuma na kupokea jumbe.

Wakenya wanahitajika kujiandikisha katika siku chini ya 45 zijazo. Kulingana naye, serikali itashirikiana na makampuni ya mawasiliano kutekeleza onyo hilo baada ya muda wa kujisajili kukamilika.

”Tutafuatilia zoezi linavyoendelea na ikifika wakati wa mwisho wa shughuli hiyo, tutaomba kampuni za mawasiliano kufunga simu zote kuzisajili upya,” alisema Bw Wangusi.

Aliambia wajumbe waliokuwa wamekusanyika Kisumu kwa maonyesho ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) mjini Kisumu.

Kulingana naye, uamuzi wa kusajili watu kidijitali ulitokana na ukuaji wa kiteknolojia nchini, na kulaumu Wakenya ambao wamepuuza shughuli hiyo.

”Baadhi ya watu wanaweza kufikiria kuwa serikali ina nia mbaya, lakini imejitolea kukabiliana na uhalifu wa kimtandao na kulinda habari za watu na siri zao,” alisema.

Alidai kuwa kuna baadhi ya watu ambao wamechukua fursa ya kujisajili M-Pesa na huduma zingine kwa kutumia majina yasiyo yao kutokana na udhaifu katika sheria.