Kimataifa

Utekaji watorosha madaktari wasio na mipaka nchini DRC

February 19th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

KINSHASA, DRC

SHIRIKA la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limesema kwamba limesitisha shughuli zote muhimu nchini DRC baada ya watu wenye silaha kuwateka nyara wafanyakazi wake wawili mapema Februari.

Wafanyakazi hao walitekwa nyara mnamo Februari 8 katika eneo la Masisi, mkoa wa Kivu Kaskazini.

Hilo huenda likawa pigo kubwa kwa taifa hilo, hasa linapojizatiti kukabili maenezi ya ugonjwa wa Ebola. “Tunasimamisha shughuli zetu DRC Kongo hadi pale wafanyakazi wetu watakapohakikishiwa usalama wao. Ni sikitiko kwamba mamlaka husika zimekosa kulinda vifaa vyetu licha ya kushambuliwa mara kwa mara,” akaeleza Francine Kongolo, aliye msemaji shirika hilo kwenye taarifa jana.Shirika hilo lilisema kwamba litarejelea shughuli zake tu, ikiwa serikali itatuma vikosi vyake kuwalinda wafanyakazi wake.Hii si mara ya kwanza kwa madaktari hao kushambuliwa na vifaa vyao kutwaliwa, ila serikali ya taifa hilo imekuwa ikiwalaumu wanamgambo kwa kupanga njama za mashambulio hayo.Shirika hilo limekuwa likiendesha shughuli za kibinadamu nchini humo kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kukabili maenezi ya Ebola tangu 2016.Mnamo 2017, shirika lilisema kwamba lilirekodi zaidi ya visa kumi vya mashambulio dhidi ya wafanyakazi wake.Hali iliendelea mnamo 2018, ila likatishia kusimamisha shughuli zote ikiwa hali hiyo haingekabiliwa.

“Tumevumilia sana wafanyakazi wetu kushambuliwa katika maeneo ambako wanatoa huduma za kibinadamu. Hata hivyo, imefikia wakati ambapo serikali ya DRC inapaswa kuchukulia rai zetu kwa uzito,” alisema Frederic Manantsoa ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo nchini humo.

Mahame

Baadhi ya maeneo ambamo limekuwa likitoa huduma zake ni Bangassou, ambapo zaidi ya watu 500,000 huwa wanalitegemea kwa huduma za kimsingi za afya.

Mara nyingi, mashambulio yanayofanywa dhidi ya vituo vyake vya afya huviacha kama mahame, bila wafanyakazi, vifaa na dawa.

Mnamo Agosti 2018 Wizara ya Afya nchini humo ilitangaza ugonjwa huo kuwa janga la kitaifa huku ikiyaomba mashirika ya kiafya na jamii ya kimataifa kuisaidia kuukabili.

Ni baada ya tangazo hilo ambapo shirika hilo liliongeza wafanyakazi wake waliokuwa wakihudumu nchini humo.Baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakiathiriwa sana na ugonjwa huo ni mkoa wa Kivu Kaskazini.