Utengano kati ya Uhuru na Ruto wadhihirika hata katika hafla ya Maombi ya Kitaifa, Safari Park

Utengano kati ya Uhuru na Ruto wadhihirika hata katika hafla ya Maombi ya Kitaifa, Safari Park

NA CHARLES WASONGA

TOFAUTI kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto zilijitokeza tena katika Hafla ya Kitaifa ya Maombi katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi, Alhamisi, Mei 26, 2022.

Wawili hao waliketi katika meza tofauti kinyume na kawaida ya hafla za awali ambapo wawili hao wamekuwa wanaketi meza moja.

Alhamisi Rais Kenyatta aliketi meza moja na Jaji Mkuu Martha Koome na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki.

Naye Dkt Ruto aliketi katika meza tofauti na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Spika wa Seneti Kenneth Lusaka, ambao wanaounga mkono azma ya urais ya Naibu Rais chini ya mwavuli wa muungano wa Kenya Kwanza (KKA).

Maaspika hao wawili ndio walikuwa wenyeji wa hafla ya maombi ya kitaifa ambayo hutayarishwa na asasi ya Bunge.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto kutoketi meza moja ni ishara ya kuzorota kwa uhusiano kati yao uliochangiwa na ukuruba wa kisiasa kati ya kiongozi wa taifa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Kwa mfano, wakati wa mazishi ya Rais mstaafu Hayati Mwai Kibaki nyumbani kwake Othaya, Nyeri, mnamo Aprili 30, 2022, Rais Kenyatta alikataa kumsalimia Dkt Ruto kwa mikono.

Katika mazingira hayo, viongozi wa kidini waliwahimiza maridhiano kati ya wanasiasa wa mirengo mbalimbali ili kutoa mazingira amani wakati wa uchaguzi mkuu.

“Tunahitaji viongozi ambao wako tayari kuondoa ubinafsi wao, ambao wako tayari kusamehe na wanaofahamu kuwa wanadamu wanaweza kufanya makossa nyakati fulani. Viongozi wanaoweka masilahi ya nchi na wananchi mbele ya masilahi yao binafsi,” Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Nyeri, Antony Muheria, akasema.

Ujumbe huo huo wa amani na umoja miongoni mwa wanasiasa ulishadidiwa na alikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Christ Is the Answer Ministries (CITAM) Dkt David Oginde na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Nchini (ACK) Jackson Ole Sapit ambayo pia walihutubu katika halfa hiyo.

Wakenya pia walitoa kauli zao katika mitandao ya kijamii kuhusu namna Rais Kenyatta na Naibu wake waliketi meza tofauti katika hafla hiyo ya maombi ya kitaifa.

“Ajabu kwamba hata katika Hafla ya Kitaifa ya Maombi Uhuru na Ruto hawawezi kuketi meza moja! Viongozi hawa wawili watenge wakati wawaelezee Wakenya kuhusu chimbuko la ukuruba wao wa kisiasa na sababu za tofauti zao,” Alinur Mohamed akasema kupitia Twitter.

  • Tags

You can share this post!

Borussia Dortmund waajiri kocha Edin Terzic

Mohamed Salah asema atasalia Liverpool msimu ujao

T L