HabariSiasa

UTEUZI: Uhuru apunguza mkate wa Ruto

July 25th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kuteua Waziri wa Leba, Ukur Yatani kusimamia Wizara ya Fedha imepunguza viti vya mawaziri wanaotoka ngome ya Naibu Rais William Ruto.

Kufuatia hatua hiyo ya Rais kuteua mrithi wa Bw Rotich kutoka Mashariki, sasa eneo hilo lina mawaziri watatu wanaotoka Rift Valley. Hao ni Simon Chelugui (Maji), Charles Keter (Kawi) na John Munyes (Madini na Mafuta).

Kwa upande mwingine wale kutoka ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya ni sita ambao ni Joe Mucheru (Mawasiliano), James Kamau (Uchukuzi), Mwangi Kiunjuri (Kilimo), Sicily Kariuki (Afya), Peter Munya (Biashara) na Margaret Kobia (Utumishi wa Umma).

Wakati walipoingia madarakani mnamo 2013, Rais Kenyatta na Dkt Ruto waligawana vyeo vikuu hasa vya mawaziri kwa maelewano na usawa, mtindo uliopendelea jamii zao.

Hatua ya jana ya Rais kuhamisha kiti hicho kutoka Rift Valley inafuata ile ya awali ambapo usimamizi wa Wizara ya Fedha, ambao tangu Jubilee kuingia madarakani mnamo 2013 ulisimamiwa na wandani wa Dkt Ruto, ulihamishwa kwa Bw Kiunjuri anayetoka Laikipia.

Bw Yatani, ambaye anatoka Marsabit, Mkoa wa Mashariki kuchukua mahala pa Henry Rotich hakuwa kwenye orodha ya waliokisiwa wangeweza kuteuliwa kwenye kiti hicho.

Kabla ya uteuzi huo jana, wadadisi walibashiri uwezekano mkubwa wa Katibu wa Wizara ya Uchukuzi, Esther Koimett kupata cheo hicho.

Hii ni ikizingatiwa kuwa amefanya kazi kwa muda mrefu katika Wizara ya Fedha, pamoja na kuwa anatoka Kaunti ya Elgeyo Marakwet, sawa na Bw Rotich.

Iwapo angemteua Bi Koimet, wadadisi wanasema Rais angeoneka lengo lake ni kufurahisha wandani wa Dkt Ruto, ambao walikuwa wakimtetea Bw Rotich.

Bw Rotich amesimamishwa kazi pamoja na Katibu Kamau Thugge baada ya kushtakiwa kwa wizi wa mabilioni ya pesa za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Rais pia alimteua Dkt Julius Muia kuwa Katibu wa Wizara ya Fedha kuchukua nafasi ya Bw Thugge, Torome Saitoti akahamishwa kutoka Wizara ya Ulinzi hadi Wizara ya Mipango, nayo nafasi yake ikapewa Meja (Mstaafu) Gordon Kihalangwa.

Kwenye uteuzi wa Bw Yatani, Rais alionyesha kukwepa siasa za ndani ya chama cha Jubilee na kuwa ana imani na balozi huyo wa zamani ambaye chama chake kilimuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Wadadisi wanasema kwa kutoteua mtu kutoka maeneo ambayo ni ngome za chama cha Jubilee, Rais Kenyatta alithibitisha kuwa anakumbatia ushirikishi katika serikali yake.

Iwapo angeteua mtu kutoka Mlima Kenya, Rais angeongeza malumbano ya kisiasa katika ya mirengo ya Tanga Tanga na Kieleweke katika chama cha Jubilee.

Wanachama wa Tanga Tanga hasa kutoka eneo la Rift Valley wangemlaumu kwa kupendelea eneo lake na kudai anapuuza eneo lao licha ya kumpiga kura kwa wingi mnamo 2013 na 2017.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Bw Yattani, aliyekuwa gavana wa Marsabit, aliongoza chama chake cha Economic Freedom Party (EFP) kuunga mkono Rais Kenyatta kuchaguliwa kwa kipindi cha pili.