Michezo

Uteuzi wa kikosi cha riadha ya AK ni wikendi hii

February 5th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MWANARIADHA Leonard Bett anatarajiwa kuwa kivutio zaidi miongoni mwa mashabiki wakati Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) litakapoanza kuteua kikosi kitakawakilisha taifa katika Mbio za Nyika barani Afrika mwaka huu. Uteuzi wa kikosi umepangiwa kufanyika wikendi hii katika uwanja wa Uhuru Gardens, Nairobi.

Bett ambaye ni mshindi wa zamani wa nishani ya fedha katika mbio za mita 3,000 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, alijumuishwa katika kikosi cha watu wazima mwaka jana. Amesema kwamba kikubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa ni kutia kapuni medali ya dhahabu katika Mbio za Nyika zitakazoandaliwa jijini Lome, Togo mnamo Aprili 2020.

Atakuwa miongoni mwa wanariadha wa haiba watakaonogesha mchujo wa kitaifa wikendi hii licha ya kuambulia nafasi ya sita katika kivumbi cha eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa kilichotawaliwa na Julius Tanki wiki mbili zilizopita.

Mashindano ya Lome yatampa Bett jukwaa la kushiriki Mbio za Nyika kwa mara ya pili katika ulingo wa kimataifa baada ya kuibuka katika nafasi ya nne kwenye kivumbi cha dunia kilichofanyika jijini Aarhus, Denmark mwaka jana.

“Japo nimeshiriki mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa muda mrefu, uteuzi wa kunogesha Mbio za Nyika ni miongoni mwa mikakati ya kuimarisha kasi na kuboresha zaidi uthabiti wangu,” akasema.

Bett aliibuka mshindi wa medali ya dhahabu katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 mnamo 2017. Hata hivyo, aliambulia nafasi ya tisa mwaka 2019 katika Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar. Mkenya Conseslus Kipruto alitetea taji lake kwa mafanikio katika mbio hizo.

Mapema mwaka 2020 Bett aliwabwaga wanariadha wa haiba kubwa kutoka humu nchini na kuibuka bingwa wa mbio za nyika za Iten Premium. Miongoni mwa watimkaji waliozidiwa maarifa na Bett ni bingwa wa mbio za kilomita 10, Daniel Simiyu.

Wakati uo huo, ujumbe kutoka Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) unatarajiwa kuwasili humu nchini wiki ijayo kutathmini kiwango cha maandalizi ya Kenya ambao ni wenyeji wa Mbio za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka huu. Mbio hizo zitafanyika katika uwanja wa MISC kati ya Julai 7-12, 2020.

Kwa mujibu wa Jackson Tuwei ambaye ni Rais wa AK, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa IAAF, Jacky Brock-Doyle ataongoza ujumbe wa maafisa 25 ambao wameratibiwa kuwasili Nairobi mnamo Februari 11 na kufanya tathmini yao kwa ushirikiano na vinara wa riadha kutoka humu nchini kwa kipindi cha siku mbili.

Ikisalia miezi mitano pekee kabla ya kufanyika kwa mbio hizo ambazo huandaliwa kila baada ya miaka miwili, ziara hiyo ya IAAF itakuwa ya nne humu nchini.

Shughuli za kukarabatiwa kwa uwanja wa Kasarani zinatazamiwa kukamilika rasmi kufikia mwisho wa Machi 2020.